Wednesday, 23 July 2014

Mbasha akana kumbaka shemejiye


NA SYLVIA SEBASTIAN
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala, jana ilisikiliza maelezo ya awali dhidi ya Emmanuel Mbasha, anayekabiliwa na shitaka la kumbaka shemeji yake.
Mbasha, alikana maelezo yote yaliyotolewa mahakamani hapo yaliyokuwa yakielezea jinsi alivyotenda kosa.
Akisaidiwa na Wakili wake, Mathew Kakamba, Mbasha alidai mahakamani kuwa hakuhusika kwenye matukio yote mawili ya ubakaji.
Mtuhumiwa huyo alikana kutenda kosa hilo, wakati upande wa jamhuri ulipokuwa unatoa maelezo ya awali jana, mbele ya Hakimu Wilberforce Luhwago.
Mbasha (32) ambaye ni mume wa  mwimbaji wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha, anadaiwa kumbaka shemeji yake (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 17.
Mapema akisoma maelezo hayo, Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, alidai Mei 23, mwaka huu, wakati mke wa Mbasha hakuwepo nyumbani, mtuhumiwa alifanikiwa kufanya mapenzi na msichana huyo.
Ilidaiwa kuwa baada ya kumbaka, alimwambia asiseme kwa mtu yeyote.
Alidai mara ya pili, Mei 25, mwaka huu, alimtaka amsindikize kumtafuta Flora, wakati wanarudi, alimbaka tena wakiwa ndani ya gari.
Wakili huyo alidai Mei 26, mwaka huu, mlalamikaji alitoa taarifa katika kituo cha Polisi Oysterbay na kupewa fomu namba tatu ya polisi (PF3) na kwenda katika Hospitali ya Amana, ambapo ripoti ya daktari ilibaini msichana huyo aliingiliwa.
Katuga alidai baada ya mshitakiwa kufahamu kuwa taarifa ziko polisi alitoweka nyumbani kwake na alikamatwa Juni 16, mwaka huu na kupandishwa kizimbani Juni 17, mwaka huu.
Hakimu Luhwago aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 22, mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikiliza upande wa Jamhuri, ambapo watakuwa na mashahidi wanne. Mshitakiwa yuko nje kwa dhamana.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru