Tuesday, 22 July 2014

Mpango mpya wa mafao wakataliwa


NA RABIA BAKARI
BAADHI ya vyama vya wafanyakazi nchini, vimepinga mchakato wa serikali ulioanza wa mapendekezo ya kuimarisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii,  unaokwenda sambamba na mapendekezo ya kupunguza viwango vya sasa vya mafao kupitia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).
Vimesema mchakato huo unakiuka haki za wafanyakazi kwa kuwa muda mrefu wafanyakazi nchini wamekuwa wakilalamikia mapato madogo kutokana na kodi kubwa inayotozwa kwenye mishahara yao pamoja na mafao duni .
Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu nchini (THTU), Yusuph Singo, walisema vyama vyao vinakubaliana kwamba kuna baadhi ya mifuko hiyo ipo katika hali mbaya kifedha, lakini suluhisho si kupunguza  malipo ya wastaafu.
Kwa upande wa Mukoba, alisema hakuna mahala ambapo vyama vya wafanyakazi na SSRA walikubaliana kwa niaba ya wafanyakazi kuhusu mchakato wa kubadili mfumo wa ukokotoaji wa mafao, hivyo vyama hivyo vinashangaa kusikia eti walikuwa na makubaliano na SSRA.
Alitaja kiwango kilichopendekezwa kupunguzwa kwenye malipo ya pensheni ya mkupuo yanayolipwa na mifuko ya PSPF na LAPF kuwa ni kutoka asilimia 50 hadi asilimia 33.3.
Aliongeza kuwa mapendekezo hayo hayakubaliki kwani viwango vya asilimia 50 ndivyo vinafaa kubakia kwa sasa.
“Mpango huu kama utatekelezwa, utapunguza kiinua mgongo cha walimu na watumishi wengine zaidi ya nusu ya kile wanachopata kwa sheria iliyopo sasa.
“Mtumishi aliyefanya kazi kwa miaka 55 na akastaafu akiwa na mshahara wa sh. 2,445,000, kwa utaratibu  wa sasa, anastahili kulipwa sh.176,855,000 kama mkupuo na pensheni ya kila mwezi kuwa sh. 950,000, lakini kwa mapendekezo mapya ya SSRA, mtu huyo atalipwa mkupuo wa sh. milioni 77,758,543 na malipo ya pensheni kila mwezi sh. 1,052,489 sawa na ongezeko la sh. 100,000,” alisema.
Alisema sababu ya mapendekezo hayo ya kuwa mifuko ipo kwenye hali mbaya, inapingwa na wafanyakazi na kuitaka serikali isitishe mpango huo na kutafuta njia nyingine ya kukabiliana na tishio lolote kwa afya ya mifuko hiyo.
Akizungumzia msimamo wa wanachama wake, Singo alisema kutokana na hali tete inayojitokeza kwenye mifuko hiyo na malalamiko ya muda mrefu ya viwango duni vya mishahara, wanatoa wito kwa wafanyakazi wote nchini kutafakari upya kama mfumo wa sasa wa uwakilishi katika masuala mbalimbali muhimu unakidhi matarajio yao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru