Monday, 28 July 2014

TEKU yatimua watatu


                                                                                    Na Solomon wansele, mbeya

WAFANYAKAZI watatu wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU), kilichopo jijini Mbeya, wakiwemo wahasibu, wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za upotevu wa zaidi ya sh. milioni 300, mali ya chuo hicho.
Upotevu huo umebainika kutokana na ukaguzi wa hesabu za chuo hicho kwa kipindi cha mwaka 2012/2013.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa upotevu wa fedha unaweza kuwa zaidi ya sh. Milioni 300 kwa kuwa hesabu za kuanzia Januari hadi Juni, mwaka huu, bado hazijafanyika.
Uchunguzi uliofanywa na UHURU umebaini wizi huo wa mamilioni hayo ya shilingi, umeibua mtafuruku mkubwa ndani ya chuo hicho huku Makamu Mkuu wa TEKU, Profesa Tully Kasimotto, akidaiwa kujaribu kulificha suala hilo.
Wakizungumza kwa masharti ya kutoandikwa majina yao, baadhi ya watumishi wa chuo hicho walisema watumishi watatu wa Idara ya Uhasibu (majina yanahifadhiwa), wameshapewa barua za kusimamishwa kazi.

"Watuhumiwa wote watatu licha ya kusimamishwa kazi, wametakiwa kuendelea kuripoti kazini kila siku, lakini hawafanyi kazi yoyote na uchunguzi zaidi unaendelea. Ni kweli kiasi hicho cha fedha kimepotea kusikofahamika, lakini kuna harufu ya kulindana katika hili,” walisema baadhi ya watumishi chuoni hapo.

Walisema fedha hizo zilizopotea ni nyingi na kwamba, zingeweza kusaidia uendeshaji wa majimbo mengine ya Kanisa la Moravian Tanzania,  inayomiliki chuo hicho.
Baadhi ya majimbo ya kanisa hilo watumishi wake wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa fedha ikiwemo mishahara ya watumishi.
Majimbo hayo mbali na lile Kanisa la Moravian Tanzania (KMT) Jimbo la Kusini, ambalo ndio mama, mengine ni Jimbo la Magharibi-Tabora, la Kusini Magharibi-Mbeya, Jimbo la Rukwa, Kigoma, Arusha na lile la Mashariki na Zanzibar.
Makamu Mkuu wa TEKU, Profesa Tully alipofuatwa na gazeti hili alishikwa na kigugumizi, kwa kujichanganya katika utoaji majibu huku akisema suala hilo bado linafanyiwa kazi, na kumtaka mwandishi asiandike habari yoyote kwani uchunguzi upo hatua za awali.
Alisema bado wanaendelea kuzifanyia kazi, na kumtaka mwandishi asubirie kwanza asiiandike habari yoyote na kuwa hata Baraza Kuu la TEKU lililokutana Julai 26, mwaka huu, lilikuwa la kawaida licha ya kuwepo kwa taarifa zenye uhakika kutoka ndani ya chuo hicho kuwa suala la wizi ndio lilitawala kikao hicho.

"Subiri hadi taarifa hizi zitakapo kuwa tayari tutazitoa kwenye vyombo vya habari...msemaji wa Chuo ni mimi hivyo nakueleza hili bado lipo katika hatua za awali kabisa, sitaki kabisa uliandike.

“Unapofanya utafiti huwezi kumtuhumu mtu kuwa ameiba fedha, labda alikosea mahesabu wewe utajuaje hilo," alisema Profesa Tully na kuongeza:

"Kusimamishwa kazi kwa watumishi hao, hakuna maana kuwa wameiba fedha hizo na kuwa hata kama hilo lipo kutokana na Chuo kumilikiwa na Kanisa, basi hata watuhumiwa wanaweza kusamehewa bila ya kufikishwa mahakamani”.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru