Tuesday, 15 July 2014

MBIO ZA URAIS 2015  •  Ngeleja naye afunguka

NA PETER KATULANDA, MWANZA
WAKATI vijana wakiendelea kupigiwa upatu katika harakati za kuwania urais katika uchaguzi mkuu mwakani, Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, ameibuka na kuweka mambo hadharani.

Ngeleja, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini na miongoni mwa wanasiasa vijana wanaotajwa kuwa wanatosha kwenye nafasi hiyo, amesema ni mapenzi ya Mungu ndiyo yatamwongoza kuwania nafasi hiyo au kuendelea na ubunge.
“Kwa sasa naendelea kutii maagizo ya Chama changu kuhusiana na suala la uraia mwakani, lakini Mungu ndiye atakayeniwezesha kufanya uamuzi wa kugombea nafasi hiyo au ubunge,” alisema wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kishinda, Sengerema wakati wa ziara ya kukagua shughuli za maendeleo jimboni kwake.
Kauli hiyo imetokana na maombi ya baadhi ya wananchi akiwemo Katibu wa CCM wa Kata ya Kishinda, Anthony Ndumila, kumwomba Ngeleja kuwania uongozi wa juu katika uchaguzi mkuu mwakani.
Huku akishangiliwa na umati uliohudhuria mkutano huo, Ngeleja alisema kwa sasa anafuata maagizo ya CCM na kwamba muda ukifika ataweka mambo hadharani.
Pia alisema baadhi ya wana-CCM wenzake wameonyesha nia ya kugombea urais, lakini anaamini jambo hilo linapangwa na Mungu na kuwa muda ukifika atasema kama ni urais au ubunge. 
“Nafahamu mpo mnaotaka nigombee urais mwakani, nawashukuru sana kwa kuonyesha imani kubwa kwangu, lakini Mungu ndiye anayepanga na kuniwezesha kuamua tena kugombea ubunge au urais,” alisema.
Tayari Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ameshatangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao. 
Pia ametoa wito kwa makada wengine wa CCM wenye nia ya kugombea uongozi huo kujitangaza mapema ili kutoa fursa kwa jamii iwajadili uwezo na utendaji wao.
Watu mbalimbali wameonyesha kuunga mkono uamuzi wa January na kutoa wito kwa vijana wengine kujitokeza huku wakidai kuwa ni wakati wa vijana kuongoza taifa.
Kuhusu maendeleo jimboni mwake, Ngelaja alisema Sengerema imepiga hatua kubwa kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba tatizo kubwa linaloikabili kwa sasa ni maji.
“Tatizo la maji ni kubwa lakini tuna bajeti nzuri katika mwaka huu wa fedha wa 2014/2015. Litapungua kwa kiasi baada ya kukamilika kwa miradi 10 ya maji ambayo vyanzo vyake vitatoka katika Ziwa Victoria, ukiwemo mradi mkubwa unaoendelea kutekelezwa mjini Sengerema,” alisema.
Diwani wa Kata ya Kishinda, Silvanus Bulapilo (CCM), alisema serikali ya CCM imechapa kazi kubwa ya kuwapatia wananchi maendeleo hivyo wasidanganyike kuchagua viongozi wa upinzani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru