NA WILIUM PAUL, MOSHI
WATU wawili wamefariki dunia papo hapo, baada ya kuangukiwa na kifusi katika machimbo ya Longoma, yaliyoko Kilema Kusini, Moshi mkoani Kilimanjaro.
Tukio hili linakuja wakati wananchi mkoani Kilimanjaro wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza ndugu zao saba waliofukiwa mwishoni mwa mwaka jana, katika maporomoko kwenye machimbo ya Pumwani, mwishoni mwa mwaka jana.
Tukio hili lilitokea juzi, saa nane mchana baada ya vijana wawili, Adrian Blessing na Shukuru Temu, wenye umri kati ya miaka 18 na 25, ambao ni wachimbaji wadogo, kuchimba nguzo zilizokuwa zikishikilia gema kubwa ambalo liliachia na kuwafukia.
Ofisa mtendaji wa Kijiji hicho, Husiwajali Kidaya, alisema vijana hao walifikwa na mauti baada ya kukaidi amri ya mmoja wa viongozi wa machimbo ya kuwataka kutoingia ndani, baada ya eneo kubwa ya gema katika machimbo kuanza kuweka ufa.
“Mwenyekiti wa wachimbaji alitoa agizo kwa vijana hawa kutoingia humu ndani kutokana na hili gema lililokatika kuonekana kuwa na ufa. Walikaidi na kuingia jana (Jumapili) kwa kuibia kwa kujua haikuwa siku ya kazi,” alisema Kidaya
Baada ya kupokea taarifa za tukio hilo, alisema alihamasisha wananchi ambao walifika na kuanza uokoaji wakiongozwa na timu nzima ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, ambapo hadi kufikia saa nne usiku, walifanikiwa kutoa mwili wa Blessing.
Alisema baadaye juhudi za kupata mwili wa pili ziliendelea ambapo jana saa 8.30 mchana, waliofanikiwa kutoa mwili wa Shukuru Temu na kwamba miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Kilema.
Kwa upande wake, Diwani wa kata hiyo, Kawawa Rudega, alisema tayari wamewasiliana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi pamoja na maofisa wa Idara ya Madini, kuhusu uwezekano wa kusitisha kwa muda shughuli za uchimbaji katika machimbo hayo.
Alisema Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Dk. Ibrahim Msengi, aliagiza machimbo hayo yafungwe mara moja huku akitoa agizo kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) kufika katika eneo hilo na kufanya tathmini ya kina kuhusu usalama wa Machimbo hayo.
Naye mmoja wa wamiliki wa machimbo katika eneo hilo, Diana Mushi, alisema kama viongozi wa eneo hilo wangekuwa waadilifu katika uamuzi kwenye mgogoro wa umiliki wa machimbo ya Longoma, maafa hayo yangezuilika.
Alisema wakati wamiliki wa Machimbo ya Longoma, wakizuia shughuli za uchimbaji katika machimbo hayo kwa kuhofia usalama wa wachimbaji, viongozi hao waliruhusu kuendelea kwa shughuli za uchimbaji.
Tuesday, 15 July 2014
Maafa mgodini
03:51
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru