Tuesday, 8 July 2014

Ridhiwani kujenga chuo cha walemavu


NA MWANDISHI WETU
MBUNGE wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, ametoa eneo la ekari 20 kwa ajili ya ujenzi wa chuo maalumu cha watu wenye ulemavu kitakachojengwa  Chalinze, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.
Chuo hicho kitajengwa na mjini Chalinze kwa ufadhili wa rafiki wa mbunge huyo aliyeko nchini Uingereza, James James, ambaye ni ana ulemavu wa ngozi.
Akizungumzia msaada huo, Ridhiwani alisema alikutana na James na kumwomba awasaidie walemavu wa ngozi katika jimbo lake ili wapate vifaa mbalimbali ikiwemo miwani na mafuta.
Hata hivyo, James alimwahidi  kwamba anaweza kusaidia zaidi kwa albino wa nchi nzima na angependa apate eneo katika jimbo hilo, ili ajenge chuo kwa ajili ya walemavu kupata elimu katika fani mbalimbali.
“Kutokana na hilo, nimeamua kutoa eneo la ardhi yangu Chalinze, ekari 20, ili ujenzi wa chuo hicho uanze. Naamini azma hii itafanikiwa na ninamshukuru rafiki yangu kwa msaada huo,”alisema.
Akizungumzia msaada huo, Diwani wa Bwilingu, Nasser Karama, alimshukuru Ridhiwani kwa kutekeleza ahadi zake katika jimbo la Chalinze.
Karama alisema wananchi wana changamoto nyingi, lakini watu wenye ulemavu wanachangamoto zaidi , hivyo ujenzi wa chuo hicho utapanua wigo wa kuwasaidia walemavu hao.
Hivi karibuni akiwa katika kampeni za uchaguzi wa jimbo hilo, Ridhiwani aliahidi kuwasaidia watu wenye ulemavu katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru