Tuesday, 15 July 2014

Katibu wa RAAWU aifagilia UPL


NA MWANDISHI WETU
KATIBU wa Chama Wafanyakazi wa Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu, Utafiti na Habari  (RAAWU), Kanda ya Mashariki, Mecki Kimoni, ameipongeza Uhuru Publications Ltd (UPL), kwa kuboresha magazeti yake ya Uhuru, Mzalendo na Burudani.
Amesema magazeti hayo yameboreshwa kwa kiwango kikubwa na kuwavutia wasomaji katika maeneo mbalimbali nchini, zikiwemo ofisi za taasisi yake.
Kimoni alisema hayo katika  kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa UPL, kilichofanyika juzi jijini Dar es Salaam juzi, ambapo alizungumzia ubora wa magazeti  kwa wasomaji na kuwataka watendaji wake kuendelea kufanya maboresho.
Alisema kumekuwa na mabadiliko makubwa ikiwemo uchaguzi wa habari zenye mvuto kwa jamii zinazoandikwa kurasa za mbele, jambo ambalo ni  mahitaji makubwa ya wateja
“Mimi ni mteja wenu.  Tunanunua magazeti haya kwa sababu yamesheheni habari zenye mvuto. Tunaomba Uhuru iendelee kuboreshwa kwa vitendea kazi ili lisambazwe kila mahali,” alisema.
Kimoni alisema Uhuru lilifahamika kwamba ni gazeti linaoandika habari za kukisifia Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini sasa linaandika habari nyingi nzuri zikiwemo za kufichua maovu yanayofanywa na viongozi  wanaokwenda kinyume cha maadili.
Alimpongeza Mhariri Mtendaji wa UPL, Joseph Kulangwa, na menejimenti yake kwa kuhakikisha vikao vya baraza vinafanyika kwa mujibu wa kanuni na sheria, kwa kuwa hilo ni eneo ambalo wafanyakazi wanajadili mustakabali wa kampuni yao.
Katibu huyo wa RAAWU, alisema ofisi yake itaendelea kushirikiana na UPL katika mambo mbalimbali. 
Katika kikao hicho wafanyakazi wa idara mbalimbali zinazounda kampuni hiyo, walijadili mambo mbalimbali ikiwemo mikakati ya kuendelea kuboresha magazeti hayo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru