NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
SHEIKH Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban bn Simba, ametangaza kuung’oa uongozi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa na ule wa Quba jijini Arusha na kutangaza uongozi mpya.
Amesema uongozi huo, utakaa madarakani hadi pale atakapofanya mabadiliko mengine ikilazimika.
Kutangazwa kwa uongozi huo, kumetengua kitendaliwa cha muda mrefu kuhusu viongozi halali wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) kwa wilaya ya Arusha na mkoa wa Arusha.
Kabla ya kutangaza uamuzi huo, Mufti Simba alisema kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro wa uongozi wa BAKWATA katika ngazi mbalimbali za wilaya na mkoa.
Alisema mgogoro huo, ulisababishwa na ukaidi wa makusudi wa baadhi ya watu katika
kukiuka taratibu za katiba kuhusu kupatikana kwa viongozi.
Kwa mujibu wa Mufti Simba, hali hiyo imesababisha uwepo wa makundi mawili ya uongozi katika ngazi moja, ikiwemo uongozi wa wilaya, mkoa, msikiti mkuu wa Ijumaa na ule wa Quba, jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya uislamu mkoani Arusha.
Alisema upatikanaji wa viongozi inaelekezwa katika Katiba ya BAKWATA ya mwaka 1999
toleo la mwaka 2008 ibara ya 10.
Mufti Simba aliutaja uongozi mpya wa BAKWATA, mkoani Arusha, ambapo Sheikh Shaaban Abdalah, amekuwa Sheikh wa mkoa huo.
Pia, Abdalah Masoud amekuwa Kaimu Katibu wa Baraza hilo, huku Mohamed Marawi akitangazwa kuwa mwenyekiti wa halmashauri ya mkoa.
Mufti Simba, aliwataja wajumbe wa Baraza la Masheikh la mkoa, kuwa ni Mwinshehe Mwinyimgeni, Nassibu Nassibu, Hussein Ijunje, Abdalah Simba na Abdulrahman Salum.
Walioteuliwa kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu wa Baraza hilo, mkoani hapa ni Hassan Salum, Said Golugwa, Athuman Yunus, Seif Banka, Athuman Luwuchu, Mohamed Laizer, Salum Majaaliwa na Rashid Msuya.
Kwa upande wa uongozi wa BAKWATA wilaya ya Arusha, Sheikh Abdulrahman Salum, ameteuliwa kuwa Sheikh wa wilaya, Mbaraka Mtonyi akiwa Katibu wa wilaya na Mohamed Marawi, akiteuliwa kuwa mwenyekiti wa wilaya.
Shaaban Maarufu, Omar Mgaza, Ayoub Juma na Hassan Mlali, walitangazwa kuwa wajumbe wa baraza la masheikh la wilaya ya Arusha.
Aidha, Ramadhan Abdulrahman, Mbega Mbega, Abdalah Mgongo, Ahmed Twarbushi, Khamis Mwalimu, Kiruwa Kiruwa, Mashaka Said, Wally Laizer, Ibrahim Munga na Abdi Nassoro, wamekuwa wajumbe wa halmashauri ya wilaya ya Arusha.
Akitangaza uongozi mpya wa Msikiti wa Ijumaa, mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Arusha, Mufti Simba alimtangaza Sheikh Shaaban Juma kuwa mwenyekiti wa msikiti na imamu atakuwa Sheikh Shaaban Juma.
Mufti Simba alimtangaza Juma Khamis kuwa Katibu wa msikiti, huku Ally Mkuruzi akiwa mweka hazina.
Wajumbe wa mamlaka ya msikiti huo, walioteuliwa ni Faraji Swai, Hassan Magire, Idd Mussa, Said Diria, Ally Iddi, Mohamed Ngeseyan, Sheha Mussa, Ahmed Omar, Rajabu Kiungiza, Jawahir Shaha, Maulid Rashid, Rashid Kapwani na Hassan Kikao.
Mbali na hao, Mufti Simba aliwatangaza wazee watano watakaokuwa na jukumu la kusuluhisha migogoro ya msikiti huo kuwa ni Mohamed Abdulrahman, Ibrahim Munga, Kasimu Mamboleo, Jaafar Wally na Hussein Bakar.
Walioteuliwa kuwa viongozi katika msikiti wa Quba uliopo Levolosi jijini Arusha ni Sheikh Hassan Waziri, ambaye amekuwa imamu na mwenyekiti wa msikiti na Abubakar Sharif amekuwa katibu wa msikiti na Chonan Jumbe kuwa mweka hazina.
Wajumbe ni Said Mwinyi, Hassan Msalu, Ghulam Mohamed, Athuman Ndosi, Ramadhan Mdoe, Issa Anzuwani, Hamza Amir, Idris Ngido na Yusuf Ngome.
Wakizungumza mara baada ya kutangazwa kwa uongozi huo, Mwenyekiti wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa, aliyeng’olewa madarakani, Abdulaziz Mkindi, alisema wao bado ni viongozi halali na wataendelea kufanya shughuli zao msikitini hapo.
Mkindi alidai Mufti Simba amevunja Katiba ya BAKWATA kwa kutangaza uongozi mpya wakati wao wapo na bado kuna kesi iliyoko mahakamani.
Alidai kutokana na hilo, watamfungulia kesi mahakamani Mufti Simba kwa ukiukaji wa Katiba.
Naye kiongozi wa masuala ya kidini katika msikiti huo, Mustafa Kiago alisema kitendo hicho cha Mufti kutangaza uongozi mpya ni sawa na kutangaza vita katika msikiti huo kwa kuwa wao
bado wapo na ni viongozi halali wakisubiri shitaka lililoko mahakamani litolewe uamuzi.
Wednesday, 2 July 2014
Mufti Simba ashusha rungu, ang’oa uongozi
08:31
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru