Wednesday 16 July 2014

Mwalimu akong’otwa kwa tuhuma za mauaji


Na Chibura Makorongo, Simiyu
MWALIMU wa Shule ya Msingi Chinamili, iliyoko wilayani Itilima, Simiyu, Festo Twange, amenusurika kifo baada ya kushambuliwa kwa silaha za jadi na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za kumuua mwanafunzi.
Mwalimu huyo alivamiwa na wananchi waliokuwa na mawe, fimbo, pamoja na mapanga kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha mwanafunzi wa darasa la tatu, Shilinde Ngíholo (12).
Kifo cha Shilinde kinadaiwa kusababishwa na kipigo kutoka kwa mwalimu huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 10:00 asubuhi, wakati mwalimu huyo akiendelea na majukumu yake ya kikazi shuleni hapo.
Siku moja baada ya madai ya mwanafunzi huyo kushambuliwa, wazazi waliamka kwa ajili ya kumtayarisha mtoto aende shule. Hata hivyo walimkuta akiwa uvunguni, amefariki dunia.
Aliongeza kuwa shangazi wa marehemu, Minza Mswahili, (48), baada ya kuona hali hiyo alikwenda kutoa taarifa ya kifo hicho shuleni.
Kwa mujibu wa Kamanda Mkombo, baada ya Mwalimu Mkuu na Mratibu wa Elimu Kata aliyekuwepo shuleni hapo kupokea taarifa hizo, walikwenda nyumbani kwa marehemu na kukuta mwili wa Shilinde ukiwa chini ya kitanda.
Baada ya walimu kuona mwili wa marehemu, Minza alianza kupiga yowe kuomba msaada wa kumkamata Mwalimu Twange kwa madai kuwa ndiye aliyesababisha kifo hicho.
ìWananchi kwa kusikia yowe walikusanyika wakiwemo mgambo wakiongozwa na Kamanda wa Sungusungu, Magambo Masele na Mtemi wa jeshi hilo, Nkindo Onyashu na kwenda kuvamia shule.
Alisema  baada ya kufika shuleni hapo, walivunja mlango katika moja ya ofisi ambayo Mwalimu Twange alikuwa amejificha na kumtoa nje kisha kuanza kumshambulia hadi kupoteza fahamu.
Hata hivyo, alisema askari polisi walipata taarifa na kuwahi kufika eneo la tukio, ambapo walikuta  Mwalimu Twange akiendelea kushambuliwa.
Kwa sasa mwalimu huyo anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Bariadi.
Akisimulia mkasa huo, mwalimu Twangwe alisema alitoka nyumbani kwake akiwa amechelewa kutokana na kumhudumia ndugu yake ambaye ni mgonjwa.
Baada ya kufika alitia saini kitabu cha mahudhurio moja kwa moja alikwenda darasani ambako alikuwa na kipindi cha hisabati.
ìBaada ya kumaliza kufundisha nilishangaa walimu wakija na kunieleza kuwa natafutwa na sungusungu kwa madai ya kumchapa mtoto na kumuua hivyo nijifiche.
ìNilijificha katika ofisi ya Mwalimu Mkuu, lakini walivunja mlango na kuanza kunishambulia hadi kupoteza fahamu na nilijitambua nikiwa hospitalini,î alisema.
Alisema kuwa madai kuwa alimchapa mwanafunzi huyo na kusababisha kifo chake si ya kweli kwani, siku hiyo, Shilinde hakufika kabisa shuleni na hata kwenye kitabu cha mahudhurio ya wanafunzi hakuwepo.
Polisi inawashikilia watu saba kwa tuhuma za kuhusika kwenye tukio hilo wakiwemo makamanda wa sungusungu, ambao wanatajwa kuhusika kumkamata mwalimu huyo.
Watuhumiwa hao ni Ngíhoro Mswahili (34), Luli Malungu (30), Minza Mswahili (48), Sanagula Sali (46), Paul Peter (28), Saba Surwa (15) na Charles Sura (62).

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru