Thursday, 10 July 2014

Ngeleja atangaza kiama kwa watendaji


NA PETER KATUANDA, SENGEREMA  
MBUNGE wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, amecharuka na kutishia kuwang’oa baadhi ya watendaji watakaokwamisha na kuchakachua miradi ya maji wilayani Sengerema.
Alisema hayo juzi alipowahutubia wananchi wa kijiji cha Busisi wilayani hapa, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na halmashauri, pamoja na kusikiliza hoja za wananchi katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Alisema hatakubali CCM ikose kura katika uchaguzi ujao kwa sababu ya watendaji wabovu wanaochakachua miradi ya wananchi kwa maslahi yao binafsi.
Huku akimpasha Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo, Barnabas Gishina, alisema: “Tuliondoa watumishi 13 walioonekana kutotimiza wajibu wao. Hatusiti kukuondoa wewe na wenzako wengine. Wananchi hawa wameguna ulipotoa taarifa ya mradi wao kwa sababu mashine yao nzima iliondolewa ikaletwa mbovu.
“Sikubali kukwamishwa na watumishi wa maji na haiwezekani kila nikija hapa ndiyo unasema mradi utakamilika baada ya siku mbili tatu, tuna dhamira njema na wananchi sisemi kwa sababu ya kuogopa uchaguzi.”
Alisema hadi sasa Halmashauri ya Wilaya hiyo kupitia Baraza la Madiwani ikishirikana na viongozi wa serikali, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na Kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya imewawajibisha watumishi 13 waliothibitika kutenda ubadhilifu wa mamilioni ya fedha za miradi ya maendeleo.
Awali, wananchi wa Busisi, wakiwemo Mayagi Mswanzari, Robert Mathayo na Shida Ngeleja chini ya Mwenyekiti wao Oswald Magesa walimwambia Ngeleja kuwa mradi huo wa maji unawapa hasara baada ya kuibwa kwa mashine ya awali na kuletewa mpya ambayo haina uwezo wa kusukuma maji kikamilifu.
Walisema mashine hiyo ilikamatwa na Mwenyekiti Oswald lakini toka ilipopelekwa wilayani Sengerema hadi sasa hawajui hatma yake na wanaendelea kupata shida ya upatikanaji maji safi na salama licha ya kua wako kando ya ziwa Victoria.
Awali, Mhandisi Gishina aisema tatizo la mashine ya chanzo cha maji Busisi ni dogo na linahitaji sh. 60,000 tu ili mradi huo uendelee kutoa huduma. Alisema bomba la kutelea maji kutoka ziwani ndilo lililoharibika kutokana na kuvunjwa na magugu maji, bila kueleza mashine yao ilivyochakachuliwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru