Thursday, 10 July 2014

Uingereza kuisaidia Tanzania mapambano dhidi ya ujangili


NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Uingereza imeahidi kushirikiana na Tanzania kuhifadhi tani 120 za pembe za ndovu zinazotunzwa nchini.
Aidha, imeahidi kusaidia harakati za Tanzania katika mapambano dhidi ya uwindaji na mapambano dhidi ya majangili.
Waziri wa Uingereza anayehusika na bara la Afrika, Mark Simmonds, alisema hatua hiyo inatokana na juhudi za nchi kukomesha uwindaji haramu.
Simmonds aliyekuwa akizungumza kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari uliohudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisifu juhudi za Rais Jakaya Kikwete kwenye mapambano hayo.
“Tunaahidi kushirikiana na Tanzania kuhifadhi na kuzitunza pembe hizo hadi pale itakapoamliwa vinginevyo,” alisema.
Alisema tangu kufanyika kwa mkutano kuhusu uwindaji haramu na biashara ya pembe za ndovu uliofanyika mwanzoni mwaka huu jijini London, Uingereza, kumekuwepo maendeleo mazuri kwenye udhibiti wa matukio ya ujangili.
Kwa mujibu wa waziri huyo, mapambano hayo yatafanikiwa kwa kuwa mkutano ulishirikisha nchi mbalimbali, ikiwemo China inayolalamikiwa kuwa soko la pembe hizo.
Waziri huyo alikuwa nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo alipata fursa ya kutembelea pori la akiba la Selous, akiambata na Waziri Nyalandu.
Kwa upande wake, Nyalandu alisema Tanzania itaendeleza mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu ili kulinda wanyama na hifadhi za taifa.
Pembe hizo za ndovu zinazohifadhiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, zinatokana na tembo wanaokufa kwa vifo vya kawaida pamoja na zile zinazokamatwa kutoka kwa wawindaji haramu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru