Tuesday, 22 July 2014

Lowassa: Utajiri wa gesi uboreshe elimu


NA MWANDISHI WETU
MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa, amesema Tanzania inaweza kutumia utajiri mkubwa wa gesi iliyogunduliwa kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu.
Lowassa  ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu, aliyasema hayo jana wakati akitoa salamu  katika Mkutano Mkuu wa 23 wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki Kati mjini Arusha.
Alisema utajiri wa gesi unaweza kutumika kuinusuru elimu kwa kuiboresha zaidi ili kuwakomboa vijana kuondokana na tatizo la ajira.
“Mwenyezi Mungu ametujalia utajiri wa gesi. Nafikiri mahali pa kuelekeza fedha za gesi ni kwenye elimu itakayokuwa bora na itakayojibu mahitaji ya sasa...huko vijijini wazazi wengi hawana uwezo.
“Tukitumia fedha hizi tunaweza kuwasaidia watu na watoto wao kupata elimu bora ya kisasa,” alisema na kuongeza kuwa elimu lazima itatue tatizo la ajira.
“Ndiyo maana kila siku nasema elimu inatakiwa iwe kwanza kilimo baadaye...mtu akipata elimu ndiyo ataweza kuendesha kilimo kwa ufanisi,”alisisitiza.
Lowassa alisema madhara ya kutanguliza kilimo kabla ya elimu ni matumizi mabaya ya matrekta ya ‘power tiller’, ambapo sehemu kadhaa yametumika vibaya kwa watu  kubeba maharusi.
Akitolea mfano Misri, Lowassa alisema wanafunzi wanaomaliza elimu ya juu ya kilimo wanapewa trekta na mkopo wa miaka mitatu kwa ajili ya kulima zabibu, kitu ambacho Tanzania inaweza kufanya hivyo.
Alisema njia nyingine ya kukabiliana na tatizo la ajira  ni kwa serikali kujenga viwanda vya nguo ambavyo vinatoa ajira nyingi na kuvikabidhi kwa sekta binafsi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru