NA SHEILA SIMBA, LUDEWA
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Rachel Kassanda, amempongeza Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, kwa jitihada za maendeleo zinazofanyika katika jimbo hilo.
Wakati Filikunjombe akipongezwa, kiongozi huyo alimshambulia Diwani wa Kata la Mlangali, Faraja Mlelwa (CHADEMA) kwa kushindwa kushiriki mbio za mwenge katika kata yake.
“Miradi saba yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni tatu katika jimbo la Ludewa ambayo mwenge unaipitia ni mikubwa. Ni wazi Filikunjombe amefanya kazi kubwa, ikilinganishwa na majimbo mengine ambayo miradi yake haifikii thamani hiyo,” alisema.
Aliyasema hayo jana, jana alipokuwa akizindua nyumba bora ya mkazi wa Mlangali Ndani, Khamis Kayombo.
Alisema mwenge umekuwa ukihamasisha maendeleo katika maeneo mbalimbali, hivyo viongozi na wapenda maendeleo, wakiwemo wabunge na madiwani, hawana budi kushiriki mbio hizo kama ilivyo kwa wananchi.
Akizungumzia kuhusu diwani wa kata ya Mlangali, Rachel alisema hata kama alikuwa na majukumu binafsi, hakupaswa kuwakimbia wananchi wake ambao walijitokeza kuupokea mwenge.
Kiongozi huyo alisema kutokana na kitendo hicho, ni wazi diwani huyo hapendi maendeleo katika eneo lake.
“Ndugu zangu Watanzania na wananchi wa Mlangali, napenda kumpongeza Filikunjombe, kwa kuwa natambua jitihada zake za maendeleo ambazo amezifanya ndani na nje ya Ludewa. Mchango wake ni mkubwa pia katika Bunge.
“Napenda kuwaeleza wazi kuwa ni viongozi wachache wa kisiasa, ambao wamekuwa wakiacha posho bungeni na kushiriki mbio za mwenge kama ilivyo kwa Filikunjombe, lakini sijapendezwa na kitendo cha diwani wenu kushindwa kufika hapa,” alisema.
Mbali na hilo, aliwasihi wananchi kuacha kuwasikiliza viongozi wa vyama vya siasa, ambao wamekuwa wakipinga mbio za mwenge, kwa kuwa mwenge si wa chama cha siasa ila upo kwa ajili ya Watanzania wote na ni sehemu ya kudumisha mshikamano, kuenzi amani na kuhamasisha maendeleo.
Thursday, 3 July 2014
Mbunge wa Ludewa amwagiwa sifa
08:43
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru