Thursday 17 July 2014

Watu 17 kortini kwa ugaidi


NA MWANDISHI WETU
WATU 17 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama za kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi na kusaidia na kuwezesha kufanyika.
Jihad Swalehe, mmoja wa washitakiwa waliofikishwa mahakamani hapo jana saa 7.20 mchana chini ya ulinzi mkali wa polisi, alisomewa mashitaka peke yake ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.
Washitakiwa wengine ni wanaohusika na mashitaka ya kula njama za kuwaingiza watu nchini na kushiriki matendo ya ugaidi ni Nassoro Abdallah, Hassan Suleimani, Anthari Ahmed, Mohamed Yusuph, Abdallah Hassan au Jibaba, Hussein Ally, Juma Sadala na Said Ally.
Pia wamo Hamis Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali, Salum Amour, Alawi Amir, Rashid Nyange au Mapala na Amir Juma.
Washitakiwa wote,  wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, waliingizwa katika chumba cha mahakama, mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa.
Baada ya kuingizwa katika chumba hicho, washitakiwa 16 walianza  kusomewa mashitaka yanayowakabili na jopo la mawakili wa serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila, akishirikiana na Mawakili wa Serikali, George Barasa, Mwanaamina Kombakono na Brenda Nick.
Akiwasomea mashitaka, Wakili Barasa alidai tarehe tofauti kati ya Januari, mwaka jana na Juni, mwaka huu,  katika maeneo tofauti nchini, washitakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa kinyume cha Sheria ya Ugaidi ya Mwaka 2002, kwa kuwaingiza watu ili wafanye makosa hayo.
Katika shitaka la pili, washitakiwa hao walidaiwa kipindi hicho na maeneo tofauti nchini, wakijua kwa pamoja, walikubaliana kuwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi zinazohusiana na vitendo vya ugaidi.
Mwangamila alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo litajwe Jumatano ijayo, kwa kuwa wanatarajia kuwa na maombi maalumu.
Hakimu Hellen aliahirisha shauri hilo hadi tarehe hiyo na kuamuru washitakiwa kurudishwa rumande.
Baada ya washitakiwa hao kumaliza kusomewa mashitaka, alipandishwa kizimbani Swalehe na kusomewa mashitaka na Wakili Brenda.
Wakili Brenda alidai tarehe tofauti kati ya Machi 21, mwaka jana na Juni 2, mwaka huu, eneo lisilofahamika mkoani Dar es Salaam, mshitakiwa alikula njama na watu wengine kutenda kosa la kusaidia kufanya vitendo vya ugaidi.
Wakili huyo alidai katika kipindi hicho, mshitakiwa kwa kujua alitumia   mtandao wa kijamii wa Facebook kwa kuwasiliana na Nero Saraiva na watu wengine ajili ya kupata malighafi, fedha na ujuzi kwa nia ya kuweka mabomu sehemu tofauti katika Jamhuri ya Kenya ili kusababisha majeraha, hofu na vifo kwa Wakenya.
Mshitakiwa hakutakiwa kujibu chochote ambapo upande wa Jamhuri, ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Hellen aliahirisha shauri hilo hadi Julai 31, mwaka huu, kesi itakapotajwa.
Washitakiwa hao waliletwa mahakamani hapo mchana wakiwa ndani ya mabasi mawili ya kubebea mahabusu huku yakisindikizwa na magari mawili ya Kikosi cha Kuzuia na Kutuliza Ghasia (FFU) na mengine matatu yaliyokuwa na askari wakiwa wamevalia kiraia.
Baada ya kusomewa mashitaka washitakiwa waliondolewa mahakamani hapo kwa kutumia basi ndogo la Magereza, wakisindikizwa na magari manne ya FFU.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru