- UVCCM yaanza kumtikisa Sugu Mbeya
- Yaapa kurejesha majimbo yote mawili
Na Innocent Ng’oko, Mbeya
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umeendelea kutikisa ngome ya mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, (Sugu) na kumtangazia kwamba CCM itarejesha jimbo hilo na la Mbozi Magharibi.
Umesema hakuna kikwazo cha kutwaa majimbo hayo kwa kuwa wananchi wameshatambua kwamba wabunge wa Chadema hawawezi kutatua kero zao na badala yake wanaendekeza maslahi binafsi.
Umoja huo umesema lengo lao kubwa ni kuizika Chadema katika majimbo yote nchi nzima ili kurejesha hatamu za uongozi za Chama cha Mapinduzi.
Viongozi wa UVCCM ambao wameuteka mji wa Mbeya kwa siku kadhaa, wamesema siri ya baadhi ya wanasiasa hao, wanaojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi( UKAWA), ni kwamba wanalipwa kati ya sh. 450,000 na 300,00 na wafadhili kutoka nje ya nchi.
Makada hao walikuwa wakizungumza katika sherehe za kuwaapisha makamanda wa UVCCM ngazi ya mkoa na wilaya katika viwanja vya Rwanda Nzovwe jijini hapa juzi.
Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM, ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Paul Makonda, alisema baadhi ya wajumbe wanaojita UKAWA, walitoka bungeni bila ya sababu za msingi na zenye tija kwa taifa.
Alisema dhana ya kupoteza muda mwingi kung’ang’ania kuwepo kwa muundo wa serikali tatu ni suala la uraia zaidi kuliko kuzingatia mahitaji ya wananchi na kwamba muundo wa serikali tatu hauwezi kuwa mwarobaini wa kutatua mahitaji ya wananchi.
Makonda alisema fedha hizo zinatolewa na mataifa makubwa yasiyo na nia njema na Tanzania na CHADEMA ndiyo inayohusika moja kwa moja na uratibu huo.
‘’Chadema kimekuwa kikihusika na uratibu wa kupata fedha hizo kutoka mataifa makubwa ili kujenga chuki, na kwamba wamesusia bunge, lakini wanalipwa posho ya sh 450,000 kwa siku,”alisema Makonda.
Makonda alihoji CHADEMA imekuwa ikipata wapi fedha za kuzunguka nchi nzima kwa helkopta, wakati wamekuwa wakilalamika hawana fedha za kufanya vikao vyao vya kikatiba na kwamba umefika wakati wananchi kuacha kudanganyika na watu wasio na nia njema na nchi.
Alisema ana ushahidi wa kutosha kuwa magari yote ya M4C ya CHADEMA yaliyosambazwa katika maeneo mbalimbali nchini, yameandikwa jina la Freeman Mbowe katika kadi za magari hayo na kwamba CHADEMA ni kampuni yenye jina la kisiasa, ambapo wananchi wanapaswa kuelewa hivyo.
Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Kagera, Hamimu Omary, alisema msimamo wa kuwa na serikali mbili umeonyesha kukidhi mahitaji ya wananchi kwa miaka 50 na kumekuwepo na ushirikiano mzuri kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.
Omary alisema katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, atahakikisha anapiga kambi mkoani Mbeya na kuhakikisha majimbo mawili ya Mbeya Mjini na Mbozi Magharibi yanarudi CCM kwa kuwa wananchi wana imani kubwa na Chama.
Alisema mahitaji ya wananchi katika mchakato wa kupata katiba mpya ni mahitaji ya kiuchumi na kwamba ni wakati mzuri kwa wananchi kuwabeza wajumbe wa katiba kutoka UKAWA, ambao wamekuwa wakirandaranda nchi nzima kutafuta huruma ya wananchi.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Ilala, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Jerry Slaa aliwataka makamanda wa vijana wa wilaya na mkoa kuhakikisha wanasimama imara katika kuwaunganisha vijana kwa kuwa ndiyo nguvu kazi ya Chama.
Alisema CCM ni Chama imara na ambacho wananchi bado wanakiamini na kwamba ni jukumu la jumuia za CCM kusimama imara na kusimamia sera na kuwaletea wananchi maendeleo.
Silaa alisema mahitaji ya mustakabali wa katiba ya nchi yanatofautiana na matakwa ya wanasiasa na wananchi kwa kuwa wanasiasa wanatumia mwanya huo kusaka maslahi binafsi.
Alisema nia ya wananchi wa kawaida ni kutaka uundwaji wa katiba unaozingatia changamoto za huduma za kijamii zinazowazunguka wananchi zikiwemo za ajira, ardhi, afya, elimu na umeme katika maeneo yao.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru