Thursday, 17 July 2014

Tanzania kuuza mahindi Kenya


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
SERIKALI imeruhusu  wafanyabishara  nchini  kuuza mahindi zaidi ya tani 200,000 nchini Kenya.,  ili kukabiliana na upungufu wa chakula uliopo nchini humo kwa sasa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Sophia Kaduma, aliyasema hayo mjini hapa jana, wakati akitia saini makubaliano hayo na Katibu Mkuu wa Kilimo wa Kenya, Sicly Kariuki.
Alisema uamuzi huo unatokana na ombi la Serikali ya Kenya, kuuziwa mahindi meupe kutokana na upungufu mkubwa wa chakula unaoikumba nchi hiyo.
Alisema utekelezaji na utiaji saini wa makubaliano hayo ni kufuatia vikao vya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Injinia Christopher Chiza na mwenzake wa Kenya, Felix Koskei, ambao walijadiliana kwa kina kuhusiana na ombi hilo.
Katibu Mkuu alisema pia serikali ya Tanzania imeona kwa kufanya hivyo, itafungua soko la wafanyabiashara nchini.
“Serikali imekubali kuuza kiasi cha tani 50,000 kutoka katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na tani 150,000 kutoka kwa wakulima. Hii ni fursa nyingine ya kufungua biashara,” alisema.
Kaduma alisema wafanyabishara watakaouza mahindi nchini Kenya watapatikana kwa njia ya ushindani na kwa mujibu wa sheria za ununuzi wa umma na watatakiwa kununua mahindi kutoka kwa wakala wa taifa.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. Batilda Burian, akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo, alisema uamuzi wa serikali kukubali ombi la Kenya unatokana na uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru