Wednesday 30 July 2014

Mfanyakazi wa ndani atoweka na kichanga



  • Mwingine aiba mtoto wa miaka miwili

NA MWANDISHI WETU, MWANZA
WIMBI la wizi wa watoto sasa limeanza kushika kasi nchini, ambapo watumishi wawili wa ndani kwa nyakati na maeneo tofauti, wametoweka na watoto wa waajiri wao.
Miongoni mwa watoto walioibwa, yupo mwenye umri wa miezi tisa na mwingine miaka miwili na nusu. Kati ya hao, mmoja amepatikana akiwa ametelekezwa barabarani.
Watumishi hao walikuwa wakiwalea watoto hao, ambapo waliofanikiwa kuwaiba wazazi wao wakiwa kwenye shughuli za uzalishaji mali.
Matukio hayo yametokea jijini Mwanza, ambapo la kwanza limetokea Ibanda, mtaa wa Nyabulogoya wilayani Nyamagana. Katika tukio hilo, mtoto Patrick Mwendesha (2), aliibwa na Vestina Odilo, aliyekuwa akimlea.
Kwa mujibu wa mama mzazi wa Patrick, Rosemary Mutakyahwa,  Vestina baada ya kutoweka na mtoto huyo bila taarifa, juhudi za kumsaka zilianza katika maeneo mbalimbali.
Alisema mapema wiki hii, Vestina alitiwa mbaroni katika eneo la Pasiansi wilayani Ilemela, alikomtelekeza mtoto huyo. Alisema wananchi walimbana na hatimaye kukiri kuwa si wake bali ni wa bosi wake.
Alipobanwa zaidi, Vestina alidai kuwa aliondoka na mtoto huyo baada ya kumlilia hivyo aliingiwa na huruma na kuamua kuondoka naye kwa kuwa amekuwa akiishi naye siku zote, hivyo amemzoea.
“Huyo mfanyakazi nililetewa na rafiki yangu anisaidie kazi za ndani. Siku  anamwiba mtoto nilimwachia kwa sababu nilishamzoea, hivyo nikaenda kujipumzisha (kulala) kidogo. Nilipoamka sikumkuta yeye wala mwanangu,” alisema.
Alisema baada ya kubaini mtumishi huyo kutoweka na mtoto, alitoa taarifa kituo cha polisi pamoja na rafiki yake ili kumsaidia kumsaka. Alifanikiwa kutiwa mbaroni na wasamaria wema.
“Alipohojiwa, alidai alimlilia hivyo akaamua kuondoka naye. Namshukuru  Mungu mtoto kapatikana. Tunawapenda wadada wa kazi, lakini tunapaswa kuwa makini na tuchunguze mahali walikotoka,” alishauri mama huyo.
Tukio lingine limetokea Jumanne ya wiki iliyopita, ambapo kichanga cha mwezi mmoja na siku saba, Aida Nuru, kiliibwa na mwananmke aliyekuwa akiishi jirani kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbugani, Bernard Wegero.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Flora Sospeter, alisema siku ya tukio, saa 12 jioni wakati akianika nguo alimwacha mwanawe na msichana huyo aliyemtaja kwa jina la Lucia Juma.
Hata hivyo, alisema baada ya kumaliza shughuli yake alikuta msichana huyo ametoweka na mwanawe.
Wegero pamoja na kuthibitisha kuwa Lucia (20) alikuwa akiishi kwake, alidai hawezi kuzungumzia suala hilo zaidi kwa kuwa ana shughuli nyingi za kusikiliza kero za wananchi wa mtaa wake.
“Mie niko bize, ninasikiliza kesi za wananchi wa mtaa wangu, njoo kesho,” alisema lakini hata alipotafutwa siku iliyofuata, alidai pia hana muda.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Christopher Fuime, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo na kusema Vestina amepandishwa kizimbani kujibu mashitaka yanayomkabili.
Kwa upande wa Lucia, alisema anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani.
Kamanda Fuime alieleza kuwa, Lucia aliyekuwa akiishi kwa Wegero akitumia jina bandia la Diana, alikamatwa juzi mjini Musoma akiwa katika harakati za kutoroka.
Hivi karibuni watoto kadhaa waliripotiwa kuibwa jijini Dar es Salaam, ambapo mtoto Meryline Repyson, aligundulika kufichwa Tandale kwa Mtogole, Dar es Salaam.
Mwizi wa mtoto huyo alikuwa akifanya mawasiliano na wazazi wa mtoto huyo akidai kulipwa fidia ya sh. milioni tatu ndipo awakabidhi.
Hata hivyo, alilipwa kiasi cha sh. 300,000 ambazo alitumiwa kwa njia ya mtandao wa simu ya mkononi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru