Tuesday 8 July 2014

Muuza nyama amuua mkewe kwa mapanga


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA.
POLISI mkoani Arusha, inamsaka muuza nyama, Lucas Lomayan (35), mkazi wa Ilboru, kwa tuhuma za kumuua mkewe kwa kumcharanga mapanga kwa kile kinachodaiwa wizi wa fedha za biashara na wivu wa kimapenzi.
Akizungumza na Uhuru, mtoto wa wanandoa hao, Jesca Lucas (10), alidai juzi saa 10 alfajiri, alisikia baba na mama yake wakizozana kuhusiana na masula ya wizi wa fedha na wivu wa kimapenzi.
Alidai baba yake alimweleza kwa ukali mama yake kuwa, alichukua fedha sh. 600,000 za biashara zake na kuzitumia kwa mambo asiyoyafahamu na kwamba ana uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine ambaye walishirikiana kula fedha hizo.
Mtoto huyo alidai alipoona wazazi wake wanafikia hatua ya kutaka kupigana, alianza kupiga kelele za kuomba msaada, ambapo baba yake alimfuata na kumtaka aache kupiga kelele na kisha alimpiga kofi la tumboni.
Alidai baada ya hapo, alimshuhudia baba yake akichukua panga (sime) na kuanza kumchoma nalo mama yake maeneo mbalimbali ya mwilini mwake huku akimtaka aeleze alikozipeleka fedha hizo na mwanaume aliyekula naye.
Alidai baada ya mama yake kukataa kutaja mambo hayo, alimshuhudia akitokwa na damu nyingi mwilini na ndipo baba yake alipoendelea kumcharanga mapanga  hadi alipoanguka chini.
Mtoto huyo alidai baada ya hapo, baba yake alitokomea kusikojulikana na yeye kuamua kwenda kwa mama yake mkubwa  kumueleza kuhusu ugomvi huo.
Alidai mama yake mkubwa alipofika eneo hilo, alimkuta mama yake akiwa amelala chini na kuanza kupiga kelele kwamba ameshafariki.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema baada ya kupata  taarifa hizo, polisi walifika eneo la tukio kwa ajili uchunguzi wa awali na kuuchukua mwili wa marehemu hadi katika Hospitali ya Mount Meru.
Alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kutoa wito kwa mtuhumiwa kujisalimisha mwenyewe polisi.
Pia, alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano katika kumsaka mtuhumiwa huyo na uchunguzi utakapokamilika watatoa taarifa rasmi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru