Thursday 3 July 2014

KASHFA YA IPTL


Kafulila aikwepa TAKUKURU

Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ameshindwa kuwasilisha ushahidi wake kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuhusiana na kashfa ya malipo yaliyofanywa na Kampuni ya IPTL kupitia akaunti ya Escrow.
Kafulila aliibua tuhuma hizo huku akiwatuhumu baadhi ya mawaziri na watendaji wa serikali, ambapo mara kadhaa serikali imekuwa ikitoa ufafanuzi kuhusiana na sakata hilo.
Hata hivyo, serikali ilitangaza kukabidhi tuhuma hizo za Kafulila kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), TAKUKURU na mamlaka zingine ili kufanya uchunguzi na kubaini ukweli.
Kutokana na hatua hiyo ya serikali, Spika wa Bunge Anne Makinda, alimtaka Kafulila kuwasilisha ushahidi wake katika vyombo hivyo ili ufanyiwe kazi badala ya kila kukicha kusimama bungeni na kuwatuhumu wengine.
Hata hivyo, hadi kufikia jana, Kafulila alikuwa hajawasilisha ushahidi huo TAKUKURU na badala yake ameishauri serikali kuchukua hatua madhubuti kuhusu sakata hilo.
Juni 25 mwaka huu, Kafulila alichafua hali ya hewa bungeni na kunusurika kuchapwa makonde kwa kumtolea kauli za kuudhi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Kafulila, ambaye alisimama bungeni na kuhoji sababu za serikali kutoa fedha hizo kupitia IPTL, alisema hakuna hukumu ya mahakama yoyote ambayo iliamrisha kufanyika kwa malipo hayo na kuhoji kwanini fedha hizo zililipwa.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azan Zungu, alimtaka Jaji Werema kutoa ufafanuzi juu ya hoja ya Kafulila, ambapo alisema fedha hizo hazikuwa za serikali na kwamba kuna taarifa potofu kuwa serikali imetoa fedha hizo kupitia IPTL, jambo ambalo si kweli na ni upotoshaji mkubwa.
Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Kafulila alisema serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhusu ufisadi wa akaunti hiyo na kwamba, wanafanya utaratibu wa kuwasiliana na UKAWA ili kulisukuma suala hilo.
Kafulila alisema ufisadi huo atauzungumza mpaka dakika ya mwisho na kwamba, yuko tayari kufungwa.
Alisema atalizungumza suala hilo kwa mapana bila ya kuogopa vitisho na kwamba, wataenda kwa wananchi kuwaeleza ukweli wa sakata hilo ulivyo.
Kwa upande wake, Msemaji wa TAKUKURU, Doreen Kapwani, alipoulizwa na Uhuru iwapo Kafulila amewasilisha ushahidi wake kama alivyotakiwa na Bunge, alisema hana hakika kama amefanya hivyo.
Awali, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambale alisema Jaji Werema amekuwa akilipotosha sakata hilo kwa kushirikiana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi.
Alisema Jaji Werema na watuhumiwa wenzake wanapotosha umma juu ya suala hilo kwamba, akaunti ya Escrow ilifunguliwa kufuatia mgogoro baina ya wabia wa IPTL.
Nyambabe alisema NCCR, inaamini kuwa akaunti hiyo ilifunguliwa na pande mbili, yaani TANESCO na serikali kwa upande mmoja na IPTL kwa upande wa pili.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru