Friday, 18 July 2014

Mh. Kamani ajenga kituo cha kutunza walemavu wa ngozi

NA PETER KATULANDA, BUSEGA.
VITENDO vya mauaji ya kikatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) wilayani Busega, vimemsukuma Mbunge wa jimbo la Busega mkoani Simiyu, Dk Titus Kamani, kuanzisha ujenzi wa kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu huo.

Kituo hicho kinachojengwa Kijiji cha Lukungu, Kata ya Lamadi, kitakachokuwa na uwezo wa kuchukua watoto zaidi ya 100, kitagharimu zaidi ya sh Bilioni 1.5.

Kutokana na jitihada za Mbunge huyo kuokoa maisha ya walemavu hao, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amemuunga mkono kwa kuchangia kiasi cha sh milioni 5 kwa ajili ya kuongeza nguvu ya ujenzi ambao tayari umeanza na unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka kesho.

Akizungumza katika eneo la ujenzi huo ambao umefikia hatua ya msingi jana, Dk Kamani alisema “Katika vitu ambavyo navifikiria sana na ningependa niondoke madarakani nikiwa nimevikamilisha, ni pamoja na kituo hiki cha walemavu.”
 

“Hapa sisikilizi la mtu lazima kituo hiki kiishe na sitaki kiwe cha ujanja ujanja, namshukuru sana mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye pia ni mlezi wa walemavu hao kuguswa na jitihada zangu na kuniunga mkono kwa kunichangia sh Milioni 5.” Alisema Dk Kamani.

Alieleza kwamba, amekuwa akijishughulisha na makundi yaliyosahaulika hasa ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambao nao ni sehemu ya jamii hivyo kituo hicho pia kitalea watoto wenye ulemavu wa viungo na macho, anaomba taasisi mbalimbali, watu wenye uwezo na wananchi wa eneo hilo wamuunge mkono ikiwa pamoja na kuwa walinzi wa watoto hao.

Alieleza kwamba, kampuni ya saruji ya Twiga ambayo imetoa mifuko 600 ya saruji iliyoanzisha ujenzi huo, imepaswa kuwa mfano bora wa kuigwa na yeye binafsi anagharamia fedha za kulipa mafundi, uchoraji wa ramani na usajiri wa kituo hicho ambacho kitaitwa Mother Thereza Albinus Disability Hope Centre.

Akielezea ujenzi huo, Mratibu wa Kituo hicho Moody Gimonge alisema kwamba, kitakapokamilika kitaanza kwa kuchukua walemavu wa wilaya ya Busega wanaolelewa katika vituo vya Shule ya Msingi Mwisenge mkoani Mara, Buhangija mkoani mkoani Shinyanga na katika sehemu nyingine za wilaya hiyo.
 

“Tuna watoto wetu walemavu wa ngozi 22 wanaolelewa Mwisenge na wengine zaidi ya hao wako Buhangija, tutaanza kwa kuwachukua kwanza hao walioko katika vituo hivyo ili vipate fursa ya kusaidia watoto wengine.” Alisema Gimonge.

Mratibu huyo alidai kuwa, anasikitishwa kuona watu wengi wanaanzisha vituo hivyo kwa ajili ya maslahi yao binafsi badala ya kuwa na dhamira ya dhati ya kuwasaidia walemavu hao kama Dk Kamani alivyo dhamiria na ni Mbunge anayetimiza ahadi yake ya kusaidia jamii ya walemavu wakiwemo Albino.
 

“Jamii iondokane na imani za kishirikina na mira potofu kwamba viungo vya Albino vinaweza kumpatia mtu utajiri wakati familia zao zilizozaa watoto hao zikiwa bado maskini hivyo kuwajengea tu vituo haitatosha bali jamii ielimike na kuchukua jukumu la kuwalinda na kuto wanyanyapaa kwani ni sawa na binaadamu wengine.” Alisema

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru