Saturday 12 July 2014

JK azindua nyumba za gharama nafuu


NA SOPHIA WAKATI, MKINGA
RAIS Jakaya Kikwete amefungua mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu wilayani Mkinga ujenzi ambao umegharimu sh. bilioni 1.4 hadi kukamilika.
Kikwete alifungua mradi huo juzi katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Rais alipongeza jitihada za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kufanikisha mradi huo huku akiitaka halmashauri ya wilaya hiyo kufanya nalo mawasiliano ili kupata nyumba zitakazowezesha watumishi wake kupata makazi.
Alisema iwapo halmashauri itafanyia kazi suala hilo kwa kuzungumza na NHC, upo uwezekano wa serikali kuu kuangalia uwezekano wa kuwaondolea kodi ya ongezeko la thamani (VAT) suala ambalo litawarahisishia kuzinunua.
Taarifa iliyowasilishwa kwa Rais Kikwete na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Felix Maagi ilisema mpango huo wa ujenzi ulibuniwa na shirika hilo katika mpango mkakati wake wa miaka mitano ulioanza mwaka 2010 ukitarajiwa kukamilika mwakani ambao unalenga kupunguza uhaba wa nyumba hasa kwa watu wa kipato cha kati na chini katika maeneo mbalimbali nchini.
Maagi alisema mpango huo wa ujenzi umekuja huku ikiwa imegundulika kuna mahitaji makubwa ya nyumba nchini ambayo yanakadiriwa kufikia milioni tatu huku kukiwa na ongezeko la nyumba 200,000 kila mwaka wakati uzalishaji ni asilimia 10 kwa mwaka mzima.
Alisema mradi huo wa nyumba 40 uliofanyika Mkinga ni mojawapo wa sehemu ya utekelezaji wao wa mpango huo wa nyumba za gharama nafuu.
Kaimu mkurugenzi mkuu huyo alisema mradi huo unasimamiwa na kutekelezwa na wataalamu wa shirika hilo, ambapo ulianza Januari mwaka jana na utakamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa mujibu wa Maagi, utaalamu uliofanyika kujenga nyumba hizo ni wa kisasa ambapo tofali za gharama nafuu zenye mchanganyiko wa udongo na saruji ambazo zimetengenezwa na mashine maalumu ya Hydroform, ndizo zilizotumika.
Alibainisha kuwa fedha za mradi huo zimetolewa na shirika kupitia mikopo kutoka taasisi za kifedha, ambapo nyumba hizozitauzwa kwa sh. milioni 40 bila VAT huku shirika likishughulikia uwekaji umeme na miundombinu ya maji na barabara katika eneo la mradi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru