Monday, 21 July 2014

Nape: UKAWA inafanya uzushi  • Asema Tume ya Katiba haikuwa ya mwisho
  •  Awataja pia Mbowe, Tundu Lissu na Jussa

Na Charles Charles
 CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetaka wananchi kujihadhari na uzushi, uongo na upotoshaji unaofanywa na genge linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ili kutaka mchakato wa Katiba mpya ukwame.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema genge hilo linafanya hivyo kutokana na uchu wa madaraka walionao viongozi wake.
Nape aliyekuwa akihojiwa katika kipindi cha Baragumu Live kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, alisema UKAWA imekuwa ikidai kuwa Bunge la Katiba halina uwezo wa kubadili kifungu chochote cha Rasimu ya Pili ya Katiba, jambo alilosema si kweli.

“Bunge (hilo) la Katiba lina mamlaka ya kile ambacho linafanya”, alisema na kuongeza: “Kilekile kinachofanyika ndani ya Bunge la Katiba ndicho kilekile kilichotungiwa kanuni na Bunge lilelile”.
Alisema kwa mfano, Kamati ya Kanuni ya Bunge hilo iliyotengeneza mwongozo wote unaotumika ilikuwa ikiundwa na wajumbe kutoka pande zote ambazo ni pamoja na CCM, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Civic United Front (CUF), Wajumbe wa Kundi la 201 na kadhalika.
Aliwataja baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo kuwa ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF ambaye pia ni mwanasheria kitaaluma, Ismail Jussa Ladhu, lakini akashangaa kuona hivi sasa nao wanazipinga.
Alilishangaa pia genge la UKAWA linapodai kuwa Bunge Maalumu la Katiba halina uwezo wa kubadili kifungu wala sura yoyote iliyomo kwenye Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba huku akihoji:
“Kama Bunge hilo halina mamlaka ya kubadili chochote hivi kwa nini tunatumia mabilioni haya ya fedha (kuligharimia) ili kufanya nini? Kwa nini watu wanatumia siku 60 wakati kumbe hawaruhusiwi kubadili kitu chochote?”
Akithibitisha kwa maandishi kuhusu uzushi, uongo na upotoshaji wa UKAWA, Nape alisoma Ibara ya 33(8) ya Kanuni za Bunge (hilo) la Katiba inayosema: “Wakati wa mjadala, mjumbe yeyote anaweza kutoa mapendekezo ya maboresho, marekebisho au mabadiliko (ya kifungu au sura yoyote iliyomo kwenye Rasimu hiyo).
“Hizi kanuni walizitunga wenyewe (ambapo ni pamoja na viongozi wa UKAWA akina Lissu na Jussa). Hii maana yake ni kwamba (chochote) kilichomo kwenye rasimu hiyo si kitu cha mwisho, (kinaweza kubadilishwa)”.
Kana kwamba haitoshi, Nape aliwashangaa baadhi ya wajumbe wa Tume ya Warioba wanaoendelea kutetea Rasimu hiyo wakati kazi yao ilikwisha, kisha akasema wanaotetea serikali tatu nao wanapigania zaidi maslahi yao kwa kusema: “Huu ni ugomvi wa madaraka wa wanasiasa”.
Akimgusia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyesema juzi, kwamba hata kama UKAWA itaendelea kususia vikao vya Bunge la Katiba, mchakato huo bado utaendelea na kuhitimishwa kwa kupigiwa kura na Watanzania wote.
Kutokana na hali hiyo, Nape alihoji sababu zinazolifanya genge hilo liendelee kufanya hivyo wakati likifahamu Bunge hilo pia si mwisho, badala yake waamuzi ni wananchi.
Alipoulizwa sababu ya Rais Jakaya Kikwete kupunga mapendekezo ya serikali tatu licha ya kufahamishwa kila hatua iliyokuwa ikifanyika wakati wa kuandika Rasimu hiyo, Nape alijibu kwamba kilichofanywa na mkuu huyo wa nchi kinastahili kupongezwa.
“Rais kama mzazi aliamua kuonesha njia, lakini mwisho wa siku uamuzi ni wako. Hata Mungu alipomuumba mwanadamu alifanya hivyo hivyo na miye nampongeza”, alisema.
Alimsifu pia kwa kuipa uhuru mpana Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kutoiingilia kwa jambo lolote, lakini akasema kauli yake kuwa Jeshi linaweza kuchukua madaraka imekuwa ikipotoshwa kwa malengo ya kisiasa.
Alisema alichofanya Rais Kikwete ni kutaka kuinusuru Tanzania ili isikumbwe na machafuko kama ilivyowahi kutokea katika baadhi ya mataifa, halafu yeye akatolea mfano wa Misri ambako mabishano ya muundo wa utawala yalisababisha nchi ipinduliwe na Jeshi.
Mchakato wa kupata Katiba mpya ya nchi umekuwa ukivurugwa na viongozi wa genge la UKAWA ambalo linaundwa na vyama vya siasa vya Chadema, CUF na NCCR – Mageuzi chini ya Mbowe.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru