Na Fadhili Abdallah, Kigoma
MWENYEKITI wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila, ameomba kuunganishwa katika kesi ya madai inayomkabili Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.
Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL), imefungua kesi ya madai dhidi ya Kafulila katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, ikiomba aamriwe kuilipa fidia ya sh. bilioni 310 kutokana na kutangaza taarifa za kashfa dhidi yao.
Katika kesi yao ya msingi, wadai hao wanaiomba Mahakama Kuu katika hukumu yake, imwamuru Kafulila awalipe sh. bilioni 210 kama fidia kutokana na kashfa hizo na hasara ya taswira ya biashara na hadhi yao.
Awali, Kafulila akizungumza kwenye mjadala katika eneo la Urusi Mwanga mjini Kigoma jana, alisema Mchungaji Mtikila ameomba kuwa mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo huku Chama chake cha DP kikiwa mshitakiwa wa tatu.
Pia alisisitiza kuwa kamwe hakukurupuka kuibua kashfa hiyo ya ufisadi katika akaunti ya Escrow na kwamba, yuko tayari kwa lolote.
“Nimefarijika kuona wenzangu wananiunga mkono katika mapambano dhidi ya ufisadi na Mchungaji Mtikila ameomba kuwa mshitakiwa wa pili,” alisema Kafulila.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Mchungaji Mtikila, alikiri kuwa amekubali kuunganishwa kwenye kesi hiyo inayomkabili Kafulila.
“Nimekubali kuunganishwa katika kesi hiyo ili kutetea haki ya wananchi wa nchi yetu kama Katiba inavyosema,” alisema.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru