Monday 21 July 2014

Mrithi wa Askofu Laizer kujulikana leo


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
ASKOFU mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, anatarajwa kupatikana leo katika Mkutano Mkuu wa 23 wa Dayosisi hiyo utakaohudhuriwa na zaidi ya wajumbe 300.
Wajumbe hao watakaokutana katika Shule ya Sekondari ya Peace House, Matevesi, Kisongo nje kidogo ya jiji la Arusha, watamchagua kiongozi atakayechukua nafasi ya Dk. Thomas Laizer, aliyefariki dunia Februari 6, mwaka jana.
Kwa sasa, nafasi hiyo inakaimiwa na Mchungaji Solomon Masangwa, ambaye awali alikuwa Msaidizi wa Askofu wakati wa uongozi wa Dk. Laizer. Mchungaji Masangwa ndiye atakayefungua mkutano huo. 

Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Samuel ole Saiguran, alisema mkutano huo mkuu utatanguliwa na ule wa Halmashauri Kuu ambao ulitarajiwa kufanyika jana jioni.
Katika taarifa yake iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Dayosisi, anayeshughulikia Misioni na Uinjilisti, Philemon Mollel, Saiguran alisema msimamizi wa mkutano huo atakuwa Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Alex Malasusa, ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani.
Alisema wajumbe wa Halmashauri Kuu walitarajiwa kukutana jana kuanzia saa mbili usiku kwa ajili ya kupokea mapendekezo ya majina ya watu watakaogombea nafasi hiyo. 
Majina yatakayopendekezwa yatapelekwa kwenye mkutano mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura. Kwa kawaida wanaopendelezwa, kwa mujibu wa kanuni ni wachungaji waandamizi na mshindi ni lazima apate zaidi ya theluthi mbili ya kura zilizopigwa.    
Wajumbe wa mkutano huo utakaomchagua Askofu ni kutoka majimbo yote ya Dayosisi ambayo ni Arusha Mashariki, Arusha Kusini, Maasai Kaskazini, Maasai Kusini na Babati.
Kwa kawaida, wajumbe halali wa Mkutano Mkuu ni wachungaji wote wa dayosisi walioko kazini, mwinjilisti mmoja kutoka kila usharika, wajumbe wawili kutoka kila usharika, wawakilishi kutoka ofisi za majimbo, wajumbe wa halmashauri kuu na wakuu wa idara za Dayosisi.
Katika hatua nyingine, Saiguran alisema mkutano huo pia utahudhuriwa na baadhi ya maaskofu wa KKKT, Askofu Mkuu Josephat Leburu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Askofu Stanley Hotay wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mlima Kilimanjaro na viongozi wa Jumuia ya Kikristo Tanzania (CCT).
Sambamba na viongozi hao wa makanisa, mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na watu mashuhuri, wakiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo na baadhi ya wabunge kutoka mikoa ya Arusha na Manyara ambayo ni sehemu ya Dayosisi hiyo. 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru