Saturday, 12 July 2014

Fedha za mfuko wa barabara wapewe wakandarasi wazawa


NA JUMBE USMAILLY, MANYONI
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amewaagiza wahandisi, mameneja wa mikoa wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha fedha zote zilizotolewa na Mfuko wa Barabara, kazi zake zote zitolewe kwa wakandarasi wazalendo.
Dk. Magufuli alitoa agizo hilo mjini Manyoni mkoani Singida wakati akiweka jiwe la msingi la barabara ya mjini Manyoni yenye urefu wa kilomita 2.8 inayotengenezwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya sh. bilioni 1.77
Alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/2015, wizara hiyo imetenga sh. bilioni 726 kwa ajili ya mfuko wa barabara.
ìNitoe wito kwa wahandisi wote Tanzania, mameneja wa Wakala wa Barabara wa mikoa yote pamoja na wakurugenzi wa halmashauri kwamba fedha zote zinazotolewa na mfuko wa barabara na hata kwenye halmashauri zote wapewe wakandarasi wazalendo.
“Kwa sababu najua nina wakurugenzi wa halmashauri hapa, zile kazi zote za sh. bilioni 726 ni lazima zitolewa kwa makandarasi wazalendo na makandarasi wazalendo na ninyi mfanye kazi kwelikweli,îalisema.
Hata hivyo, Dk Magufuli hakusita kumkingia kifua mkandarasi wa barabara hiyo kwa kutomaliza kwa wakati kazi yake, kwamba kilichochangia sio yeye bali ni wizara kutomlipa fedha anazodai kwa mujibu wa sheria.
ìWatu walipomuona mkandarasi anatengeneza madaraja wakaanza kusema mkandarasi huyu hafai na kama watu hawafai sifai mimi kwa sababu sijamlipa hela, lakini mkandarasi anafaa na ndiyo maana kwa makusudi mazima nimekuja kuweka jiwe la msingi hapa.
ìNa nataka nikuhakikishie mkandarasi najua unadai sh. milioni 600, serikali ya Rais Kikwete ni tajiri, fedha hizi tutakulipa ndani ya wiki mbili kuanzia leo (juzi), lakini na wewe uanze kufanya kazi usiku na mchana barabara hii iweze kumalizika, wananchi wa Manyoni wanataka lami,î alisema.
Awali katika taarifa ya TANROADS Mkoa wa Singida, Mhandisi Leonard Kapongo, alitoa changamoto zinazoikabili miradi mikubwa miwili iliyopo kuwa ni madeni ya zaidi ya sh. bilioni 80 zinazodaiwa na wakandarasi wa barabara ya Manyoni -Itigi - Chaya na daraja la mto Sibiti.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru