Wednesday 23 July 2014

Sumaye: Kuna tishio la matajiri na masikini kutoelewana


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, amesema kuna tishio la kutokea kutoelewana baina ya matajiri na masikini nchini.
Amesema hali hiyo inaweza kusababisha vurugu nchini kama hatua hazitachukuliwa mapema ili kunusuru hali hiyo.

Amesema katika jamii, kuna chuki inayotokana na tofauti kubwa ya kimapato baina ya makundi tofauti, hasa kati ya matajiri wachache na wenye madaraka kwa upande mmoja na masikini walio wengi kwa upande wa pili, ambavyo husababishwa na mfumo mbaya wa uchumi na ubinafsi uliokithiri usiojali wengine.
“Hali hii ni ya hatari kwa amani na utulivu wa taifa lolote kwa sababu walio wengi hawatavumilia kuona watu wachache wakiishi katika anasa za kutisha wakati walio wengi hawamudu hata mahitaji ya lazima kwa maisha. Hapa kwetu hali hii ipo na ni dalili isiyo nzuri, hivyo inahitajika kudhibitiwa kwa haraka kabla haijaleta madhara makubwa kwa taifa letu,” alifafanua Sumaye.
Aliyasema hayo katika salamu zake wakati wa mkutano mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati uliofanyika Sekondari ya Peace House mjini Arusha.
Sumaye alisema suala la umoja ni muhimu kwa kuwa bila umoja, hakutakuwa na nguvu na mshikamano na kila mmoja atajifanyia lake analolijua bila kujali kama lina athari gani kwa mtu mwingine, lakini mwisho wa yote wote watakuwa dhaifu.
Aliongeza kuwa siku hizi hata katika uchaguzi wa nafasi za uongozi kwenye nyumba za ibada, hujitokeza tabia ya watu kujitenga na viongozi waliochaguliwa, kwa sababu tu huyo aliyechaguliwa hakuwa chaguo lao, hali ambayo huwafanya viongozi kuongoza kwa shida.
“Kiongozi anayechaguliwa na wengi ndiye kiongozi wetu sote, hata wale ambao hatukumpigia kura. Ni lazima tuwe na umoja baina yetu sisi wenyewe na tuwe na umoja baina ya sisi na viongozi wetu, na pia umoja baina yetu sisi na binadamu wenzetu ambao tunaishi nao. Hapo ndipo tutakapofurahia matunda ya umoja wetu, yaani upendo, amani na maendeleo,” alisema Sumaye.
Alitoa mfano kuwa kuna nchi ambazo zimeingia katika hali ya uvunjivu wa amani, hata kupigana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu hakuna umoja baina ya watu wake na kila upande ukipigania kuudhulumu mwingine au kunakuwa na chuki zimejengeka baina ya pande zinazohusika.
“Katika siasa, tofauti hizi huweza kutokea pale ambapo upande mmoja huhisi kuwa unadhulumiwa au unaonewa katika maamuzi ya kisiasa, hasa nyakati za kampeni, upigaji kura na wizi wa kura.
“Wakati mwingine hali hii hutokea kwa upande mmoja kukataa tu kushindwa hata kama wameshindwa kwa halali,” alisema na kusisitiza kuwa, jambo hilo la kisiasa limeleta fujo katika nchi nyingi za Afrika na kusababisha umwagaji wa damu.
Aliongeza kuonya kuwa, eneo lingine la hatari ni la chuki za kidini au zinazotokana na imani za watu ambalo vita vyake vibaya zaidi na huishia kuuana bila kuwa na mshindi.
Katika mkutano huo, Sumaye alimpongeza Askofu Mteule, Mchungaji Solomon Massangwa, kwa kuchaguliwa kuwa Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati kujaza nafasi iliyoachwa wazi na marehemu Askofu Dk. Thomas Laizer.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru