Tuesday 15 July 2014

Dk. Mwinyi akiri ugaidi ni tishio


NA MOHAMMED ISSA
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, amesema ugaidi na uharamia ni changamoto kubwa kwa nchi za Afrika Mashariki.
Amesema matatizo yanayotokea Somalia yanatishia usalama wa nchi za Afrika Mashariki na kwamba juhudi zinapaswa kuchukuliwa kudhibiti hali hiyo.


Dk. Mwinyi alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua maonyesho ya majeshi ya nchi kavu.
Alisema matukio ya kigaidi na kiharamia yanayojitokeza kwenye nchi mbalimbali duniani, yanasababisha changamoto kubwa za kiusalama  kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.
Dk. Mwinyi alisema matukio hayo yanatishia usalama wa nchi mbalimbali duniani na kwamba yasipodhibitiwa yanaweza kusababisha athari.
“Matukio ya ugaidi na uharamia bado ni changamoto kubwa kwa nchi zetu, tunapaswa tuyadhibiti ili yasijitokeze kabisa,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, matukio ya yanayojitokeza nchini Somalia nayo ni tishio kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisema matukio hayo yanasababisha vifo na uharibifu wa mali na kwamba nchi za Afrika Mashariki zinapaswa kujipanga kudhibiti matukio ya aina hiyo.
Dk. Mwinyi alisema katika kongamano hilo, watajadili mambo mbalimbali ya kiusalama yanayozikabili nchi za Afrika Mashariki.
Alisema baada ya kumalizika kongamano hilo, watataweka mikakati mbalimbali itakayoziwesha nchi hizo kujiimarisha kiulinzi na usalama. Pia alisema hilo ni kongamano la kwanza kufanyika nchini na limeshirikisha nchi za Afrika Mashariki.
Katika kongamano hilo, kulikuwa na maonyesho ya zana mbalimbali za kijeshi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru