Tuesday, 22 July 2014

Dengue yaua watu 25,000 kila mwaka


Na Selina Wilson
WATU 25,000 wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na ugonjwa wa homa ya dengue ulioenea katika nchi 110 duniani, ikiwemo Tanzania.
Hayo yalisemwa jana mjini Dar es Salaam na Mtaalamu wa Udhibiti na Ufuatiliaji Magonjwa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Geofrey Mchawa, katika mafunzo ya siku moja ya waandishi wa habari za afya kuhusu ugonjwa wa dengue.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa watu 50 hadi 390 wanaambukizwa ugonjwa huo kila siku duniani na kwamba kwa hapa nchini, wapo waliougua na kupoteza maisha
Hata hivyo, alisema bado hakuna chanjo wala tiba ya kutibu virusi vya ugonjwa huo,
badala yake mgonjwa hutibiwa magonjwa yaliyojitokeza baada ya kuambukizwa dengue.
Alisema mara nyingi mgonjwa hutibiwa homa kwa dawa za kutuliza maumivu kama vile paracetamol na kwamba hatakiwi kupatiwa dawa kali zinazoweza kuleta madhara.
Akizungumzia hali ya ugonjwa huo nchini, Dk. Vida Makundi, alisema katika kipindi cha wiki moja sasa, hakuna mgonjwa aliyeripotiwa kuugua ugonjwa huo.
Dk. Vida alisema ugonjwa wa dengue ulisababisha vifo vya watu wanne, akiwemo daktari mmoja kabla ya wizara kuchukua hatua za kuudhibiti.
Alisema ugonjwa huo huambukizwa na mbu aina ya aedes, mwenye virusi vya dengue kwa kumng’ata mtu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru