NA RABIA BAKARI
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema haitoongeza muda wa kuandikisha Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo mpya wa BVR, licha ya wanasiasa wengi kupendekeza.
Aidha imetoa ruksa kwa vyama vyote vya siasa vinavyohitaji kuweka mawakala kufanya hivyo wakati wa uandikishaji wa daftari hilo.
Mapendekezo ya kuongeza muda kutoka siku 14 hadi mwezi au miezi miwili, yalitolewa juzi na viongozi wa juu wa vyama vya siasa, walioshiriki mkutano kati yao na NEC kwa ajili ya kujadili maboresho ya daftari hilo.
Walisema kutokana na uzoefu uliopo wakati wa uandikishaji wa daftari la mwanzo, na upungufu uliojitokeza, ni wazi muda uliopangwa na NEC hautatosha.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Malaba, alisema jana kuwa muda wa siku 14 unatosha kwa kuwa kabla hawajafikia hatua ya kutangaza, walifanya utafiti wa kutosha.
“Tulishaeleza kwamba muda wa siku 14 unatosha kabisa, maana tulifanya utafiti wa kutosha na isitoshe kuandikisha mtu mmoja, hakutachukua hata dakika 10 kwa jinsi mfumo ulivyo. Na zaidi tumeongeza vituo na hivyo kumfikia kila mmoja anayetakiwa kupiga kura kwa mujibu wa sheria,” aliongeza.
Kuhusu ombi la kuweka wakala, alisema wameruhusu kwa vyama vyote vya siasa vyenye kujiweza kufanya hivyo, kwa kuwa si mara ya kwanza kuwa na mawakala wakatiwa uandikishaji wapigakura.
Malaba aliongeza kuwa mafunzo ya kutumia vifaa vitakavyotumika kuandikishia wananchi, yatatolewa kwa viongozi wote wa vyama vya siasa na wadau wengine ambao ni wahusika wa hatua hiyo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru