Thursday, 3 July 2014

Werema aliteleza - Bomani


NA RABIA BAKARI
SAKATA la Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, kuchukizwa na kauli za kuudhi za Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila na kutaka kumchapa makonde, limechukua sura mpya.
Tukio hilo ambalo lilichafua hali ya hewa bungeni, limekuwa likivuta hisia za watu wengi, ambapo limemuibua Jaji Mstaafu Mark Bomani na kusema kuwa, Jaji Werema aliteleza.


Alisema kwa wadhifa na majukumu mazito ya Jaji Werema ndani ya Bunge, hakupaswa kutoa maneno makali wala kujibizana na Kafulila ndani ya bunge na kwamba, anachoamini ni kuwa mwanasheria huyo aliteleza.
Jaji Bomani, ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mjini Dar es Salaam, jana, kuhusiana na masuala mbalimbali, ikiwemo mchakato wa Katiba Mpya.
Katika majibizano hayo, Jaji Werema alipandwa na hasira baada ya kuitwa mwizi na Kafulila, ambapo naye alijibu mapigo hayo huku akitumia fasihi.
“Wanyankore wanasema tumbili hawezi kuamua kesi ya msitu, hivyo naomba nisikilize hata kama nina makosa we nisikilize kwanza,” alisema Jaji Werema kwenye mjadala huo, na kutafsiriwa kwamba alimuita Kafulila ‘Tumbili’.
“Ukiwa kiongozi hutakiwi kuwa na jazba na uwe tayari kutukanwa, hivyo Jaji Werema hakutakiwa kupandisha hasira, alitakiwa kujizuia na nadhani katika hilo aliteleza,” alisema Jaji Bomani.
Alitumia fursa hiyo kuwaonya viongozi wa ngazi mbalimbali wa serikali, kuhakikisha wanakuwa makini na ndimi zao ili kuepuka kujitumbukiza kwenye dimbwi la uhuni.
Hata hivyo, alisema anaamini kupitia kwa Jaji Werema, viongozi wengine watakuwa wamejifunza na watakuwa makini.
Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, hususan mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba, alisema mjadala ulianza vibaya kwa wajumbe kutoleana lugha chafu na kashfa mbalimbali na kwamba, iwapo wangepewa muda zaidi, hali ingekuwa mbaya.
Kutokana na hilo, alishauri hoja ya muundo wa serikali kuwekwa kando ili wajumbe wapate fursa za kujadili vipengele vingine muhimu vilivyopo katika Rasimu ya Pili ya Katiba.
“Kumekuwa na mabishano makali kuhusu muundo wa serikali, kwa sasa kipengele hicho kinaweza kuwekwa pembeni na mambo mengine muhimu yakaendelea kujadiliwa,” alisema Jaji Bomani.
Hata hivyo, alisema kamwe Katiba Mpya haiwezi kupatikana kwa malumbano au kuhesabu kura na kwamba, ni lazima nchi iendelee kusonga mbele.
“Hata kama hatutapata muafaka na kutopata Katiba mpya, bado sio mwisho wa dunia. Nashauri waweke kando hoja hizo na kujadili mengine. Muda mwafaka ukifika wa kuridhiana basi watarejea kwenye kipengele cha muundo wa serikali,” alisema na kuongeza: “Kuna wenzetu waliochukua muda mrefu hadi kupata Katiba… Kenya iliwachukua miaka 10 na kuna nchi yamezuka mapigano na hadi damu kumwagika. Sisi hatupaswi kufika huko ni hatari kwa taifa.”
Aliwataka wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kurejea bungeni kuendelea na mjadala ili kuokoa mabilioni ya fedha za umma.
“Nawaomba hata UKAWA warudi bungeni wajadili mambo mengine. Kuna mambo mengi ambayo hayahitaji malumbano na yanaweza kuingia kwenye Katiba bila hata kuhitaji kura za maoni, tusikwamishwe na idadi ya serikali,” alisisitiza.
Alisema haamini kama ipo siku ngumi zinaweza kuibuka katika vikao vya bunge nchini kwa kuwa huo si utamaduni wa kitanzania.
Aliwasihi wajumbe wakirudi katika Bunge Maalum la Katiba, kuzingatia muda kwani, gharama ni tatizo lingine linaloweza kukwamisha mambo mbalimbali ya maendeleo nchini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru