Monday 21 July 2014

CPA kuwa ya kimataifa?


Na Mwandishi Wetu, Arusha
KAMATI ya wawakilishi wa mabunge wanachama  wa Jumuia ya Madola Kanda ya Afrika (CPA) inatarajia kuwasilisha ripoti yenye mapendekezo ya kutaka Bunge hilo liwe na mwonekano wa kimataifa.
Ripoti hiyo itawasilishwa katika mkutano mkuu wa 45 unaofanyika mjini Arusha.
Uamuzi wa kuwasilishwa kwa ripoti hiyo ulifikiwa jana na kamati ya wawakilishi wa mabunge wanachama wa umoja huo,  iliyoketi katika ukumbi wa mikutano kwenye hoteli ya  Ngurdoto.
Akizungumza katika kikao cha kamati hiyo kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Seneta Letapata Makhaola wa Lesotho,  ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya  CPA Kanda ya Afrika, Katibu Mkuu wa CPA, Dk. Thomas Kashilillah, alisema ripoti hiyo inatokana na mapendekezo ambayo timu ya wataalamu wa sheria walipewa na kutakiwa kuyafanyia utafiti.
Matokeo ya utafiti huo unatoa hali halisi inavyotakiwa kuwa katika mabadiliko hayo.
Alisema ripoti hiyo itawasilishwa kabla ya kufunguliwa rasmi kwa mkutano keshokutwa, ili kutoa nafasi kwa wajumbe kuijadili na kutoa mapendekezo ya mabadiliko hayo.
 “Ripoti hiyo itawasilishwa katika mkutano huu 45 na makubaliano yatakayofikiwa yatawasilishwa kwa maspika wa mabunge wa nchi wanachama, ambao wataombwa kuyawasilishwa kwa wakuu wa nchi mapendekezo ya mabadiliko,” alisema Dk. Kashilillah.
Umoja wa Mabunge wa Jumuiya za Madola Kanda ya Afrika umefikia hatua ya kutaka kufanya mabadiliko katika muundo wake wa sasa wa taasisi ya hiari, iliyosajiliwa chini ya sheria za Uingereza.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru