Wednesday, 23 July 2014

UFISADI VYAMA VYA USHIRIKA


JK: Hatutabeba mizigo ya wezi

  • Aagiza vigogo kufikishwa kortini haraka
  • Aonya fedha za umma sio za kuchezewa

Na Mwandishi Wetu, Tunduru
RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali haitalipa madeni ambayo baadhi ya Vyama vya Ushirika nchini vinadaiwa na benki.
Amesema anataka kwanza wezi waliosababisha madeni hayo wakamatwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Aidha, Rais Kikwete amesema ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya maofisa wa serikali hujidhalilisha kwa kujifanya mawakala wa wanunuzi binafsi wa mazao ya wakulima, hasa wakati wa msimu wa ununuzi huo.
Pia amewataka wana-ushirika nchini kuacha kuwachagua wezi kuongoza vyama vyao, vinginevyo itafikia hatua vyama hivyo vitakufa kabisa.
Aliyasema hayo juzi wakati alipohutubia mkutano wa hadhara na wakati alipozungumza na viongozi wa mkoa huo, ambapo aliyakataa maombi ya wananchi wa Tunduru, ambao waliomba serikali ikilipie deni la sh. bilioni 2.6, ambalo Chama cha Ushirika cha TAMCU kinadaiwa na mabenki.
“Nasikitika kuwajulisheni kuwa siko tayari kuidhinisha chama chenu kilipiwe deni mpaka ithibitike deni hilo lilitengenezwa vipi kwa sababu huko nyuma tumepata kulipa madeni yote ya Vyama vya Ushirika kwa kiasi cha kati ya sh. bilioni 27 na 30. Nataka kupata maelezo ya uhakika jinsi chama chenu kilivyopata deni hilo – je ni hasara ya kawaida ama ni wizi tu wa viongozi wa chama hicho,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Serikali haiwezi kubebeshwa deni la wezi. Sharti langu kwenu na kwa uongozi wa mkoa wa Ruvuma ni kwamba kwanza wakamatwe wezi hao na kufikishwa mbele ya sheria na ndipo tuzungumzie kama tunaweza kulipa deni hilo pamoja na kujua ukweli kwamba, serikali ndiyo ilidhamini vyama vya ushirika kukopa. Kazi ya serikali haiwezi kuwa ni kutumia pesa ya umma kulipa madeni yaliyosababishwa na watu wanaochonga line na kutengeneza madeni. Hatuwezi kufidia wezi.”
Aliongeza: “Kazi kuu ya Vyama vya Ushirika ni kulinda wakulima kwa sababu hivi ni vyama vyao, tena vyama vya hiari. Hivyo, ndiyo walikuwa wanafanya akina Mzee Kahama wa BCU, akina marehemu Bomani wa Victoria na wale wa KNCU. Sasa vyama hivyo vimekuwa sehemu ya kuwadhulumu wakulima.
“Sasa hata viongozi wa ushirika nao wamekuwa mawakala wa wanunuzi binafsi. Hata maofisa wa serikali nao wamo. Wanashinda wanazunguka vijijini huko wakati wa msimu kuwafanyia kazi wanunuzi binafsi. Ni jambo la kusikitisha. Hii ndiyo inaeleza kwa nini mfumo wa Stakabadhi Ghalani umekuwa na maadui wengi kwa sababu maadui hao ni pamoja na maofisa wa Serikali.”

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru