Wednesday 9 July 2014

TRA yazuia gari la Naibu Waziri



  • Adaiwa kukwepa kulipa kodi kwa miaka miwili

Na Latifa Ganzel, Morogoro
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imekamata gari la Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, kwa tuhuma za ukwepaji kodi.
Habari za kuaminika na zilizothibitishwa na Meneja wa TRA Wilaya ya Mvomero, Hemed Leso, zimesema kuwa Makalla anadaiwa kodi ya leseni ya barabara ya sh. 662,500.
Imeelezwa kuwa gari hilo aina ya Toyota Dyna lenye namba T534 BFP, lilikamatwa wakati wa operesheni ya kuwasaka wakwepa kodi iliyoendeshwa na maofisa wa mamlaka hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Leso alisema katika operesheni hiyo iliyosimamiwa na Kampuni ya Udalali ya Yono Action Mart, magari kadhaa yalikamatwa likiwemo la Makalla.
Alisema baada ya kukamatwa kwa magari hayo, wahusika walijulishwa, akiwemo Makalla, ambaye alidai kuwa hatalipa kwa kuwa gari lake lilikamatwa kihuni.
“Tulifanya mawasiliano na wahusika, lakini Makalla kupitia namba ya simu ya kiganjani (namba zinahifadhiwa), akatujibu akisema halipi kwa sababu mazingira ya kukamatwa kwa gari lake yalikuwa ya kuhuni na hiyo inaonyesha jinsi raia wanavyopata taabu kwa kuwa watu wanakamata magari bila vitambulisho,” alisema akinuu ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwa Makalla.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Morogoro, Kilomba Kanse, alipoulizwa alisema tayari amepokea malalamiko hayo.
Alisema nyaraka za usajili wa gari hilo zinaonyesha kuwa mmiliki wake ni Gabriel Amos Makalla na kwamba, linadaiwa kutolipiwa kodi hiyo kwa miaka miwili.
Alisema kodi ya leseni ya barabara ya gari hilo imefikia kikomo chake Februari 8, mwaka jana.
Kanse alisema operesheni hiyo ya kusaka wakwepa kodi ilifanyika mkoa mzima na kwamba, haikulenga mtu mmoja.
Makalla alipotafutwa kuzungumzia sakata hilo, hakuweza kupatikana huku simu yake ya kiganjani ikikatwa kila inapopigwa.
Wakati huo huo, Makalla kuanzia Julai 3 hadi 7, mwaka huu, alifanya ziara ya kikazi iliyolenga kuhamasisha shughuli za maendeleo ya wananchi wa  vijiji vya tarafa za Mlali, Turiani na Mvomero.
Katika ziara hiyo, alitoa misaada ya kifedha na vifaa kwa ajili ya kuharakisha  maendeleo ya huduma za kijamii, ikiwa ni pamoja na kuzindua vituo vya maji Mgogo, kata ya Sungaji, kijiji cha Mlali na Kipera, kutoa misaada ya kifedha kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali, vijana , taasisi za dini na ujenzi wa ofisi za CCM kata na matawi.
Kwa mujibu wa maelezo yake, sehemu kubwa ya misaada ya kifedha ilielekezwa kwenye sekta ya elimu ili kusaidia uendelezaji wa ujenzi majengo ya madarasa ya shule za awali na mikondo ya madarasa ya kwanza kwenye vijiji vya tarafa hizo baada ya wananchi kuonyesha nguvu zao wakiwa na lengo la kuwaondolea adha watoto wanaotembea umbali mrefu kwenda shule.
Mbunge huyo pia akiwa Mji Mdogo wa Dakawa, alikabidhi msaada wa vyakula, ambako alitoa tende katoni 50 na mchele tani 1.5 kwa ajili ya waumini wa dini ya kiislamu ambao wako kwenye mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan wilayani humo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru