Na Ally Ndota, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeonya viongozi na watendaji wake kuacha tabia ya kuwabeba wana-CCM wanaotangaza nia ya kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao, kwani kufanya hivyo ni kukiuka kanuni na miongozo ya Chama.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai ametoa onyo hilo alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kamati za Siasa za Mkoa na Wilaya za Kichama za Mjini na Amani, ikiwa ni mfululizo wa ziara ya wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya NEC, Zanzibar.
Alisema CCM inaongozwa kwa kanuni na taratibu zinazotambulika kikatiba, hivyo hakitomvumilia mwanachama anayevunja kanuni hizo kwa maslahi yake binafsi kwani kila jambo limewekewa utaratibu ambao unapaswa kufuatwa na kila mwanachama.
Alifafanua zaidi kuwa kila mtu ndani ya Chama anayo fursa ya kugombea nafasi za uongozi, lakini hana budi kufuata utaratibu, kwani kuna watu wameanza kuwatumia baadhi ya viongozi wa Chama kuwapigia kampeni za chini kwa chini wakati muda wa kufanya hivyo bado haujawadia.
“Ni marufuku kwa mwana-CCM kuanza kutangaza nia ya kugombea nafasi yoyote hasa urais, ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi au udiwani kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, kwani muda wa kufanya hivyo bado haujafika,” alisema Vuai.
Aliwaagiza viongozi hao kuelekeza nguvu zaidi katika kubuni mbinu na mikakati madhubuti, ikiwemo kujipanga kikamilifu kwa madhumuni ya kuwaandaa watu wenye sifa za kupiga kura ili waweze kuleta ushindi wa kishindo kwa Chama katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Pia, aliwataka kufanya kila linalowezekana kuhakikisha majimbo matatu ya Mtoni, Magogoni na Mji Mkongwe yanakombolewa kutoka Chama cha CUF na kuwa chini ya himaya ya CCM.
Kwa upande wao, wajumbe hao walisisitiza kuendeleza suala zima la umoja na mshikamano miongoni mwao na kuacha tofauti zao pale zilipojitokeza ili waweze kutekeleza kikamilifu Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, kwa maslahi yao, vizazi vyao na taifa kwa ujumla.
Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar, wamekamilisha ziara katika mikoa mitatu ya kichama ya Kaskazini, Kusini na Mjini, Unguja.
Wednesday, 23 July 2014
CCM: Marufuku kutangaza nia ya kugombea urais
08:08
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru