Thursday, 3 July 2014

Kasi ya kupambana na ngoma za vigodoro iongezwe


NA MOHAMMED ISSA
 HIVI karibuni Jeshi la Polisi lilipiga marufuku ngomo za usiku maarufu kwa jina la vigodoro.
Ngoma hizo huchezwa kwenye sherehe mbalimbali na huvutia watu wa rika tofauti ambao hufika kuangalia na wengine kucheza.
Mara nyingi, vigodoro hupigwa kwenye maeneo ya nje ya mji, na kukusanya kundi kubwa la watu.
Sehemu inayopigwa vigodoro hutokea matukio mengi yakiwemo ya vurugu na uhalifu huku watu wakicheza uchi hususan wanawake.
Hivyo, baada ya polisi kufuatilia kwa muda mrefu wamebaini ngoma hiyo haifai kwa sababu za kiusalama na kudhibiti ukiukwaji wa maadili unaofanywa na baadhi ya wanawake ambao hucheza uchi wa mnyama bila kujali.
Binafsi naunga mkono agizo hilo la polisi la kupiga marufuku vigodoro, sioni umuhimu wa ngoma hizo. 
Kwenye vigodoro kunafanyika matukio mengi ya aibu ambayo hayaendani na maadili ya Kitanzania. 
Si jambo la kushangaza kuona baadhi ya wanawake wakisagura nguo zao hadharani bila ya aibu yoyote, hufanya hivyo mbele ya watoto, ndugu zao na hata wazazi wao.
Naomba jamii tuliunge mkono Jeshi letu la Polisi kwa kupiga vita vigodoro kwenye maeneo yetu ili kudhibiti matukio ya kihalifu yanayoweza kujitokeza.
Pia ninaliomba jeshi la polisi, kufuatilia kwa makini agizo hilo kwani kwenye baadhi ya mitaa vigodoro vinaendelea kupigwa.
Mbali  na hilo, polisi wafanye doria kwenye baa ambazo zinaruhusu wahudumu wa kike kuvaa mavazi ya nusu uchi ili kuvutia wateja.
Tukio hilo nililishuhudia hivi karibuni, maeneo ya Yombo baada ya kuingia kwenye baa moja maarufu eneo hilo ambapo wahudumu wake wanavaa mavazi yasiyoendana na maadili ya Kitanzania.
Kwa kweli nilishangazwa sana na mavazi ya wahudumu hao, ni ya aibu kwani asilimia kubwa ya mwili uko uchi.
Nilipojaribu kuulizia kwa nini wanavaa hivyo nilielezwa kuwa, wanafanya hivyo ili kuvutia wateja na ili msichana aweze kufanya kazi katika baa hiyo ni lazima akubali kuvaa mavazi ya aina hiyo.
Kama kweli jeshi la polisi limedhamiria kukomesha vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya Mtanzania, linapaswa kufanya operesheni maalumu kwenye baa ambazo zinakiuka utamaduni wa Mtanzania na wasisite kuwachukulia hatua kali za kisheria wahudumu na wamiliki wa baa hizo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru