NA LILIAN JOEL, ARUSHA
WAJUMBE wa Halmshauri Kuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, wamependekeza jina moja la mchungaji Solomon Massangwa kuwa Askofu wa kanisa hilo.
Uamuzi huo ulifikiwa juzi usiku katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Peace House iliyoko kata ya Matevesi wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa, jina la Mchungaji Massangwa, ambaye alikuwa Kaimu Mkuu wa Dayosisi hiyo, ndilo lililopendekezwa na kikao cha Halmashauri Kuu na kupelekwa katika mkutano mkuu wa 23 wa Dayosisi wenye wajumbe 300 kwa ajili ya kuthibitishwa.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk. Thomas Laizer, ambaye alifariki dunia Februal 6, mwaka jana, baada ya kuugua ugonjwa wa shinikizo la damu katika hospitali ya rufani ya Selian iliyoko Arusha.
Vyanzo vya habari viliendelea kusema kuwa, majimbo matano ya Dayosisi hiyo ya Arusha Mashariki, Arusha Magharibi, Maasai Kusini, Maasai Kaskazini na Jimbo la Babati, yote yalipendekeza jina moja la Mchungaji Massangwa kurithi kiti hicho alichokiacha marehemu Askofu Laizer.
Habari zilisema kutokana na hali hiyo, kikao cha Halmshauri Kuu cha Doyosisi hiyo kiliamua kwa kauli moja kupeleka jina moja katika mkutano mkuu huo ili kuthibitishwa.
“Tumeazimia kupeka jina moja la Mchungaji Massangwa katika mkutano mkuu, ambalo linaonekana kupendekezwa na majimbo yote matano mkuu ya dayosisi yetu,” kilisema chanzo chetu.
Aidha chanzo hicho cha habari kilisema kuwa, kazi kubwa itakayofanyika katika mkutano huo mkuu ni kupitisha jina la Masangwa kwa kuwa ameonekana kuwa chaguo la majimbo yote matano na hakuna malalamiko yeyote yaliyopatikana.
“Tunashukuru Mungu wachungaji wote wameonekana kuridhika na jina hilo bila kuonyesha dalili zozote zile kuwa wamebaguliwa kwa njia moja au nyingine katika mchakato uliofanywa na majimbo yote, wote wanaonekana kuridhika,”alisema mtoa taarifa wetu.
Awali, wajumbe wa mkutano huo walionekana kuwa na shauku kubwa ya kusubiri majina yatakayoletwa katika mkutano huo kwa lengo la kupigiwa kura.
Mkuu wa wilaya ya Arusha, John Mongella, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, alisema serikali inatambua mchango wa kanisa katika kusaidia jamii, hasa katika nyanja za kijamii.
Alisema matarajio ya serikali ni kuona kuwa, mrithi wa marehemu Askofu Laizer atakuwa sio tu kiongozi wa kanisa, bali ni kiongozi wa jamii husika .
Hadi gazeti hili linakwenda mtamboni, jina la Mchungaji Massangwa bado lilikuwa halijapata baraka za mkutano huo mkuu kuwa askofu wa Dayosisi hiyo
Tuesday, 22 July 2014
Massangwa apendekezwa kumrithi Askofu Dk. Leizer
08:14
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru