Wednesday, 30 July 2014

Waliokula fedha za WAZAZI matatani


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
JUMUIA ya Wazazi Tanzania, imeahidi kupeleka timu ya wakaguzi wa hesabu ili kubaini chanzo cha madeni yanayoikabili Shule ya Sekondari ya Leguruki, mkoani hapa. 
Madeni hayo yanatokana na na baadhi ya watumishi waliojinufaisha na fedha za shule hiyo na kisha kutoroka na kuiacha ikiwa na madeni lukuki.
Katibu wa Wazazi Mkoa wa Arusha, Daniel Mgaya, alisema tayari makao makuu ya jumuia wameshakubali kutuma timu hiyo baada ya kumalizika kwa sikukuu ya Idd el Fitri. Aliwaomba watumishi wa shule hiyo kutoa ushirikiano kwa timu hiyo itakapofika shuleni hapo.
Alisema kabla ya ufisadi uliofanywa na baadhi ya watumishi,  shule hiyo ilikuwa na uwezo wa kujiendesha pasipo kutegemea mchango wowote kutoka nje, hivyo kusisitiza  kwamba hawatakuwa tayari kuona  ikiadhirika wakati inajulikana wazi watu walioifikisha mahali hapo.
Pia aliwatoa wasiwasi watumishi wa shule hiyo pamoja na wazazi juu ya uvumi kuwa shule imeshindwa kujiendesha na kwamba iko katika hatua za mwisho za kufungwa.
“Wazazi pamoja na walimu wangu msiwe na wasiwasi shule hii haifungwi, endeleeni kuchapa kazi na leteni watoto wenu. Ninachowaahidi  baada ya ya sikukuu hii tutatuma timu kukagua hesabu. Haiwezekani watu waibe fedha halafu wapite mitaani kutangaza shule imekufa na inafungwa,” alisema Mgaya.
Awali, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mtambo wa umeme wa jua shuleni hapo uliogharimu sh. milioni 55 kupitia ufadhili wa shirika la Energy Assistance la Ubeligiji, Mkuu wa Shule hiyo, Emanuel Loyi, alisema shule imekuwa ikishindwa kujiendesha kutokana na deni sugu la zaidi ya sh. milioni 24.
Alisema madeni hayo ameyarithi kutoka uongozi uliopita tangu mwaka 1991 ambayo ni yale ya makato ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) yaliyosababisha kufungiwa kabisa. 
Loyi aliuomba uongozi wa jumuia kupitia mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa wa Arusha, Bernard Murunya, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Taifa, Abdallah Bulembo, kuandaa hafla  ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kulipa madeni hayo na mambo mengine, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa mabweni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru