Tuesday, 15 July 2014

Halmashauri zamwagiwa mabilioni kuimarisha afya


NA WILLIAM SHECHAMBO
HALMASHAURI nchini zitanufaika baada ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupatiwa sh. bilioni 108 na wadau wa maendeleo ya afya, kwa ajili ya kuboresha huduma katika sekta hiyo.
Katika fedha hizo sh. bilioni 80.4 zimetengwa na serikali kutoka kwenye fungu hilo ili ziende kwenye halmashauri nchini kwa lengo la kufanikisha mpango wa afya wa mwaka katika halmashauri husika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, alisema hayo jana Dar es Salaam na kueleza kwamba fedha hizo zimetolewa wakati muafaka.
Alisema pamoja na halmashauri, uongozi wa afya ngazi za mikoa pia utanufaika kwa kupatiwa sh. bilioni 3.8 huku sh. bilioni 15.3 zikielekezwa kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Dk. Likwelile alisema sehemu zote ambazo fedha hizo zimegawanywa zinahusika moja kwa moja na kufanikisha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG) ikiwemo kudhibiti vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
Alisema kutokana na wizara kupewa kipaumbele na serikali hata kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), wataendelea kuchapa kazi kadri ya uwezo wao kwa ushirikiano na wadau wa afya.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donald Mmbando, alisema wamejitahidi katika kupambana na magonjwa kadhaa ikiwemo Dengue, ambapo kulikuwa na vifo vinne na wagonjwa 1,300.
Alisema kwa sasa wameelekeza mikakati kamambe kuhakikisha ugonjwa wa Ebola haufiki nchini.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru