- Serikali yazijia juu Tambaza na Iyunga
NA MOHAMMED ISSA
SERIKALI imesema imechukizwa na matokeo mabaya ya kidato cha sita kwa sekondari za Tambaza Dar es Salaam na Iyunga, Mbeya.
Imesema kutokana na matokeo hayo katika shule hizo kongwe za serikali nchini, imetoa mwezi mmoja kwa walimu wakuu kujieleza sababu za kufanya vibaya kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini, alisema hayo ofisini kwake mjini Dar es Salaam, jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wanafunzi waliofaulu masomo ya sayansi.
Alisema matokeo mabaya waliyopata wanafunzi wa shule hizo yameisikitisha serikali kutokana na shule hizo kuwa na vifaa na walimu wa kutosha.
“Haiwezekani uwe na shule ina kila kitu halafu ifanye vibaya, tumewapa wahusika mwezi mmoja watupatie maelezo ya kina kabla hatujachukua hatua,” alisema.
Alisema shule zote zilikuwa na sababu ya kufanya vizuri kutokana na kuwa na nyenzo za kufundishia, wakiwemo walimu wa kutosha.
Sagini alitolea mfano shule ya Sekondari ya Iyunga, ambapo alisema ina walimu wasiopungua 70 wanaofundisha masomo mbalimbali pamoja na vifaa vya kutosha vya kufundishia.
Alisema shule ya Tambaza ilishawahi kufanya vizuri, lakini wameshangazwa na matokeo ya mwaka huu yamesababishwa na nini.
Shule hizo zilikuwa miongoni mwa shule kumi zilizofanya vibaya katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa hivi karibuni.
Sagini alisema katika matokeo ya mtihani wa mwaka huu, yanaonyesha kuwa wanafunzi 22,685 kati yao wasichana 7,859, wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi.
Alisema ufaulu wa watahiniwa wa shule kwa mwaka jana, katika madaraja ya kwanza mpaka ya tatu umeongezeka kwa asilimia 100.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru