Wednesday, 2 July 2014

Mwakyembe awang’oa vigogo 13 kwa rushwa


NA MOHAMMED ISSA
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amewatimua vigogo 13 kutoka wizara mbalimbali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Vigogo hao kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Afya na Ustawi wa Jamii, wamerejeshwa kwenye wizara zao kwa hatua zaidi za kinidhamu na kisheria.


Pia ametoa onyo kali kwa watumishi wengine uwanjani hapo wenye tabia za kujihusisha na rushwa kuwa, hakuna atakayebaki salama, ni lazima atakutana na mkono wa sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Dk. Mwakyembe alisema vigogo hao wamekuwa na tabia za kuomba rushwa na kubughudhi abiria.
Aliwataja vigogo waliong’olewa kuwa ni Teddy Masenga, Ester Kilonzo, Rehema Mrutu, Mery Kadokayosi, Kisamo Samji na Aneth Kinanga, wote kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Wengine ni Agness Shirima, Hamis Bora, Valery Chua na Midus Kakulu, ambao wanatoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Watumishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ni Eshi Samson na Anne Setebe.
Kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe, watumishi hao wamebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuwabugudhi abiria mara kwa mara.
Alisema abiria kutoka nchi za Falme za Kiarabu na China, wamekuwa wakilalamika kukaguliwa tofauti na abiria wengine, jambo ambalo limeelezwa kuwa ni katika kutengeneza mazingira ya rushwa.
Dk. Mwakyembe alisema abiria hao wanadai wanapoingia na vyakula, wananyang’anywa na watumishi hao na ili waweze kurejeshewa, wanatakiwa kutoa kati ya Dola za Marekani 50 mpaka 150.
“Wengine wanapoingia wanatakiwa kuwa na kadi ya homa ya manjano na wanapokuwa hawana, badala ya kupigwa sindano, wanaombwa rushwa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” alisema Dk. Mwakyembe huku akionyesha kukasirishwa na hali hiyo.
Pia, alisema baadhi ya watumishi walioondolewa uwanjani hapo, wamebainika kuzuia bila sababu hati za kusafiria za abiria wanaoingia nchini hadi wapewe chochote ndipo huzirejesha.
Alisema kutokana na malalamiko hayo, aliwaomba watu wa usalama kumpatia taarifa ya uhalifu unaofanywa na watumishi mbalimbali uwanjani hapo.
Dk. Mwakyembe alisema taarifa alizopatiwa zinahusisha picha zilizopigwa na kamera za siri (CCTV), ambazo hutumika kurekodi matukio yanayofanywa na baadhi ya watendaji kila siku.
Alisema baada ya kupatiwa picha hizo, watumishi hao wameonekana wakiwasumbua abiria kwa kuwatishia na wengine wakionekana kupokea rushwa.
Dk. Mwakyembe alisema yuko tayari kuzitoa picha za watumishi hao iwapo, watalalamika kuwa wameonewa ili kuufahamisha umma ukweli wa mambo.
“Kama kuna mtu ataona ameonewa katika hili, ajitokeze hadharani na nitathibitisha hilo kwa kutoa picha hizi ili kila mmoja aweze kuziona. Leo (jana) nimeamua kuwa mstarabu, lakini kama watalalamika tu nitazitoa hadharani,” alisisitiza.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha maeneo yote ya viwanja vya ndege nchini yanakuwa salama na hakuna usumbufu unaojitokeza.
Waziri huyo alisema watumishi hao walikuwa hawavai sare kama watumishi wengine na kwamba walikuwa wakivaa mavazi ya nyumbani.
Alisema kuanzia sasa mtumishi ambaye havai sare, atatolewa nje ya uwanja huo na hataruhusiwa kuingia tena.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru