NA FRANK KIBIKI, IRINGA
BARAZA la Maaskofu Tanzania (TEC), limeitaka serikali kuhakikisha wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wanarejea bungeni bila masharti.
Limesema Bunge Maalumu la Katiba lipo na linaendeshwa kwa mujibu wa sheria hivyo, wajumbe wanapaswa kurejea pindi litakapoanza vikao vyake ili kuutendea haki mchakato wa Katiba Mpya.
Hata hivyo, limeonya kuwa iwapo wataendelea kukaidi, wananchi wasiwachague tena kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwani, watakuwa wameshindwa kuonyesha uwajibikaji.
Hayo yalielezwa jana na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Askofu Severine Niwemugizi, wakati akitoa salamu za baraza hilo katika Jubilei ya kutimiza miaka 25 ya Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa.
Katika Jubilei hiyo, Waziri Mkuu Mkuu, Mizengo Pinda, alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Askofu Ruyemugezi alisema kitendo cha UKAWA kutoka bungeni ni kukiuka Katiba ya nchi na kukwamisha mchakato huo, hivyo wananchi wanapaswa kuwaadhibu kwa kuwasaliti.
“Bunge lipo kisheria na wanapaswa kuwakilisha maoni ya wananchi, sasa wasiporejea wananchi wasiwarudishe tena kwenye nyadhifa zao za uongozi wakati wa uchaguzi mkuu mwakani.
“Kutoka nje ya Bunge ni kuwasaliti wananchi kwani, maoni ya rasimu hiyo yatakuwa ya watu wachache, jambo litakalowalazimu wananchi kujitokeza kupiga kura ya kuikataa.
“Suala la Katiba mpya lisiachwe kwa wanasiasa badala yake maoni ya Watanzania na Tume ya Katiba yaheshimiwe ili ipatikane katiba itakayotufikisha miaka 50 ijayo,” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika marekebisho ya daftari la kudumu la wapigakura litakapokuwa likirekabishwa ili watumie haki yao ya msingi ya kuwachagua viongozi bora.
Pia, alitumia fursa hiyo kuitaka serikali kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumiwa na Watanzania wote ili kudhibiti hali mbaya ya kuibuka kwa matabaka ya matajiri na masikini.
Naye, Waziri Mkuu Pinda alisema serikali imepokea wito wa Baraza hilo la kuwataka UKAWA warejee bungeni, mara bunge hilo litakapoanza ili Katiba itakayojadiliwa iwe kwa maslahi ya watanzania wote na sio wachache.
Aliwataka UKAWA kurudi ili wakabishane ndani ya bunge na kufikia muafaka huku wakitafakari nchi ilikotoka, ikiwa na serikali mbili zilizo ndani ya taifa moja.
Aliwasihi viongozi wa dini kuendelea kuwalea na kuwaimarisha waumini kimaadili kwa madai kuwa, ikiwa familia, jamii, dini na serikali watashirikiana kwa pamoja, maovu yaliyopo hivi sasa yatapungua.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma na wakuu wa wilaya zote za mkoani hapa.
Tuesday, 1 July 2014
‘UKAWA rudini bungeni’
09:00
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru