Tuesday 1 July 2014

Usultani waitesa CHADEMA



  • Mwigamba aibuka tena, ampongeza Msajili
  • Katibu, viongozi wa kata tisa waachia ngazi

Na waandishi wetu
TUHUMA za ubabe na usultani wa baadhi ya viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), bado umeendelea kukitesa na kukipasua vipande chama hicho. 
Hatua hiyo imetokana na baadhi ya viongozi, akiwemo Mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe, kupigwa ‘stop’ kuwania tena nafasi hiyo baada ya kubainika Katiba ya CHADEMA imechakachuliwa ili kuondoa kipengele cha ukomo wa viongozi.
Tayari Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imesema Katibu Mkuu Dk. Willibroad Slaa na Mbowe hawana sifa za kugombea tena uongozi wa chama hicho kwa kuwa Katiba haiwaruhusu.
Hatua hiyo imetokana na malalamiko yaliyowasilishwa na baadhi ya wanachama wa CHADEMA, akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wake mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Mwigamba alisema ukweli kuhusu ubabe na usultani ndani ya CHADEMA umedhihirika.
“Nashukuru Mungu ukweli wa mambo ndani ya CHADEMA sasa umedhihirika. Nilitukanwa na kupewa majina yote mabaya, lakini demokrasia na uhuru niliokuwa naupigania umeonekana,” alisema Mwigamba.
Alisema alibaini kuwa viongozi wamechakachua Katiba ya CHADEMA baada ya Mbowe kujitokeza hadharani na kuanza kupambana na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe aliyekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuongoza chama hicho, katika nafasi ya uenyekiti.
Alisema kwa mujibu wa katiba, Mbowe hakuwa na sifa za kuendelea kugombea kwa kuwa alishafikia ukomo wa uongozi, hivyo alipofuatilia alibaini vipengele vimebadilishwa  kinyemela bila kushirikisha vikao halali.
Alisema baada ya kubaini hilo, viongozi wa juu walianza kumdhibiti ikiwa ni pamoja na kumvua nyadhifa zake ili asiingie kwenye vikao vya maamuzi.
“Nilianza kuwekewa mizengwe ya kila aina, nikatafuta muhtasari wa vikao kadhaa, lakini sikuona vipengele vilivyobadilishwa kuhusu uongozi. Ila Katiba iliguswa kipengele hicho hivyo, kwa kushirikiana na wenzangu, tukapeleka malalamiko kwa msajili kwa hatua zaidi,” aliongeza Mwigamba ambaye kwa sasa ni mwanachama wa ACT Tanzania.
Mwigamba alisema baadhi ya wanachama hususan vijana hawakumwelewa wakati akipigania haki hiyo na wengine walitumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kumdhihaki.
“Nikiwa kituo changu cha Arusha, nilikuwa naona mambo kawaida, lakini nilihamia makao makuu ndipo nikaona hiki chama kinaendeshwa kiajabu. Hakiwezi kushika dola wakati kimejaa uozo na kukiuka misingi na taratibu zake,” alisema na kuongeza:  “Viongozi ni wabinafsi, wanajijali wenyewe hivyo nikaanza kupigania mabadiliko ili tuweze kusonga mbele”.
Alisema mwisho wa CHADEMA utafika baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya Mdhibiti Mkuu na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu mapato na matumizi ya chama hicho.
Alisema kuna ufisadi mkubwa ndani ya CHADEMA, ambapo fedha za umma zinazotolewa kama ruzuku, zimekuwa zikitafunwa na wachache na hakuna hesabu zinazoeleweka.
Wiki iliyopita baadhi ya wanachama wa CHADEMA, wakiwemo wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu, waliandamana na kuwasilisha malalamiko dhidi ya viongozi wao kwa msajili na CAG. 
Huku wakiwa na mabango, wajumbe hao walitaka ofisi hiyo kuubana uongozi wa CHADEMA kuhusu kukiuka Katiba na matumizi mabaya ya fedha za ruzuku na madaraka.
Hata hivyo, kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, amekuwa akiwaponda kuwa ni mamluki na kuwa wametumwa na CCM. 
Naye Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, alisema vyama vya upinzani nchini vinajitahidi kuikosoa serikali, lakini vyenyewe vimeoza.
Alitolea mfano baadhi ya wabunge wa CHADEMA waliodai kuwa Katiba ya Tanzania imekaa kisultani, huku wakificha usultani ulioota mizizi ndani ya vyama vyao.
“Hata hao wanaosema wanaweka mazingira ya wengine kugombea uongozi, bado vikwazo ni vingi,
hata wanachama kuogopa kujitokeza na watu wanapita bila kupingwa. Kabla ya kulaumu ni vyema tukajiangalia wenyewe kwani, nyumba zetu ni chafu,” alisema.

Wasomi waponda
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mohammed Bakari, amesema vyama vya upinzani vinaweza kusambaratika kutokana na usultani uliokithiri.
Alisema vyama hivyo vinapaswa kuiga sera na mipango kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambazo ndizo zinakifanya kuendelea kutawala kwa miaka mingi.
Alisema vyama vingi vya siasa vilianzishwa na watu ambao wamekuwa wakitumia umaarufu wao kung’ang’ania madaraka na kwamba, ndio sababu ya migogoro ya mara kwa mara.
Kuhusu uamuzi wa Ofisa ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Bakari alisema ni mwafaka na anauafiki kwa kuwa vyama hivyo vilianzishwa kwa sheria namba nne ya mwaka 1992 na lazima ifuatwe.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Alli, alisema uamuzi wa msajili ni mtihani kwa CHADEMA na wanapaswa kuangalia namna ya kuumaliza.
Alisema vyama vingi vya siasa vinakosa sura ya utaifa na migogoro inayotawala ndani ya vyama hivyo inaweza kuvisambaratisha.
Alisema vyama vingine ukiacha CCM, vimekuwa havifanyi vizuri katika kubadilisha nafasi ya mwenyekiti.
Bashiru alisema mgogoro wa CHADEMA ulianza tangu enzi za marehemu Chacha Wangwe na umeendelea na kuhamia kwa Kabwe.
“Vyama hivi havifanyi vizuri katika kubadilisha mwenyekiti na vimekuwa vikikabiliwa na migogoro hata wakati wa kuteua wagombea katika uchaguzi. Kwa kiasi kikubwa vingi vinakabiliwa na ukiritimba wa demokrasia,” alisema.

Katibu wa Jimbo, vigogo wa kata tisa waachia ngazi
Katika hatua nyingine, CHADEMA imeendelea kusambaratika baada ya Katibu wa Jimbo la Mpanda Mjini, Joseph Mona na viongozi wa kata tisa za wilaya ya Mpanda, kuachia ngazi.
Viongozi hao walibwaga manyanga juzi na kuweka hadharani kuwa, majungu na udikteta wa viongozi wa juu umewashinda.
Wakizungumza baada ya kutangaza kuachia ngazi na kujivua uanachama, viongozi hao walisema uendeshaji holela wa chama hicho, ikiwemo matumizi mabaya ya fedha ni miongoni mwa mambo yaliyowakimbiza.
Mona aliliambia gazeti hili jana kuwa, alishindwa kuendelea kuliongoza jimbo hilo kwa sababu viongozi wake ni wababe na hawashauriki.
Alitaja majina ya kata ambazo wenyeviti na makatibu wake walijiuzulu juzi kuwa ni Ilembo, Kasamlili, Makanyagio, Misunkumilo, Shamwe, Kakese, Kawajense na Mpanda Hoteli.
“Tunapiga kelele za kutaka mabadiliko kwenye serikali, lakini ndani ya taasisi yetu kumeoza na hakutamaniki. Chama kinaendeshwa kwa hisia, ikionekana mwanachama anataka mabadiliko anafukuzwa,” alisema Mona na kuongeza: “Jimbo letu lina mbunge, lakini katika kipindi cha miaka tisa tumepewa ruzuku ya sh. milioni 16 tu ila kila mwezi tunaletewa fomu za marejesho, sasa hizo fedha zinakwenda wapi.”
Naye Wastara Feruzi, ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jimbo la Mpanda Mjini, alisema sababu za kujiuzulu ni kuchoshwa na majungu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru