Tuesday, 1 July 2014

Dk. Mwakyembe kuweka mambo hadharani leo


Na mwandishi wetu
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameahidi kuwataja hadharani baadhi ya watumishi na watendaji wanaofanya vitendo vya uhalifu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.


Awali, Dk. Mwakyembe, alikuwa akutane na waandishi wa habari ofisini kwake jana, lakini alishindwa kufanya hivyo baada ya kuitwa Ikulu kwa majukumu mengine ya kikazi.
Hatua ya kuwekwa hadharani mtandao huo hatari  unaohusisha watumishi wa idara mbalimbali, inafuatia agizo lake alilitoa kutaka taarifa za uhalifu unaofanywa na baadhi ya watumishi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kuwa maofisa wa vikosi vya ulinzi na usalama uwanjani hapo  wamekamilisha jukumu hilo na kukabidhi taarifa  kwa Dk. Mwakyembe.
Taarifa hizo zinahusisha picha zilizopigwa na kamera za siri (CCTV) ambazo hutumika kurekodi matukio yanayofanywa na baadhi ya watendaji kila siku.
Habari zilisema katika baadhi ya picha hizo, wataonekana  vigogo hao wakiwasumbua abiria kwa kuwatisha, huku wengine wakipokea mlungula au kutoa lugha chafu.
Licha ya kupata uhakika wa kukabidhiwa kwa picha hizo, Uhuru haikufanikiwa kupata majina ya vigogo waliorekodiwa  wanaohusishwa na rushwa.
Maofisa hao walifanikisha kukamatwa kwa raia wa Oman akiwa na dawa za kulevya na kutaka wahongwe sh. milioni 20 na gari ili wamwachie.
Dk. Mwakyembe alisema anachukizwa na kuwepo kwa watumishi wasiokuwa na uadilifu ambao wamekuwa wakiwasumbua wageni pindi wanapowasili kwa kujivika majukumu ambayo si yao.
“Nafahamu kila kitu kinachoendelea. Nakuagizeni nipeni taarifa za picha zote zinazowaonyesha watumishi wakichukua rushwa na kuiba marashi ya wageni wakati wa ukaguzi na picha zao nitaziweka katika vyombo vya habari,” alikaririwa akisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru