Tuesday 1 July 2014

Meneja EWURA alijinyonga-Polisi


NA MWANDISHI WETU
JESHI la Polisi limesema hakuna anayetiliwa shaka kuhusiana na kifo cha aliyekuwa Meneja Udhibiti wa Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Julius Gashaza kwani alijinyonga.
Gashaza alikutwa amekufa kwa kile kilichodaiwa kujinyonga kwa kutumia tai katika nyumba ya kulala wageni ya Mwanga, eneo la Yombo Vituka, mjini Dar es Salaam.
Meneja huyo alikuwa amefariki dunia  siku moja baada ya kurejea kutoka Dodoma kikazi Mei 18, mwaka huu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili kuhusiana na matokeo ya uchunguzi wa tukio hilo ambalo limegubikwa na utata.
Hata hivyo, alisema kinachochunguzwa ni kufuatilia kiwango cha hasira kilichosababisha ajinyonge kilitokana na nini na hivyo kazi hiyo bado haijakamilika.
Alipoulizwa ni lini uchunguzi huo utakuwa umekamilika, Kamanda Kiondo alisema hawezi kuweka muda kwa kuwa uchunguzi unahitaji kufuatilia mambo mengi.
‘Hatuwezi kueleza ni lini uchunguzi utakamilika kwa tukio la mtu kujinyonga, hatuwezi kujua tufanye uchunguzi kwa muda gani.
“Hakuna mtu anayetiliwa shaka, hivyo tunafuatilia kwa nini alipata hasira hadi akajinyonga na nani alisababisha,” alisema.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipoulizwa kuhusu uchunguzi wa tukio hilo alisema, uchunguzi bado haujakamilika.
Kifo cha Gashaza kilichotokea Mei 18, mwaka huu, baada ya kutoka Dodoma kukutana na Kamati ya Bunge ya Bajeti, iliyowaita maofisa wa EWURA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kujitokeza tofauti ya takwimu za mafuta yaliingizwa nchini na kutozwa kodi.
Kwa mujibu wa taarifa, takwimu zilionyesha tofauti ya TRA na EWURA ni sh. bilioni 25. 
Katika kikao hicho,  Gashaza alikwenda kumwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi na aliporejea Dar es Salaam, hakufika nyumbani kwake na badala yake alikwenda kulala hotelini ambako siku iliyofuata alikutwa amejinyonga.
Habari zaidi juu ya tukio hilo zilieleza kuwa kilitokana na utata na kwamba tofauti hiyo ya hesabu ilikuwa ni lita 11,755,161, ambazo zingeuzwa kwa bei ya sasa ya petroli mkoani Dar es Salaam ya sh. 2,200 zingepatikana sh 25.86 bilioni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru