Tuesday, 1 July 2014

Majengo ya ghorofa yatishia maisha Dar


NA MWANDISHI WETU
WAMILIKI wa baadhi ya majengo wamekiuka amri iliyotolewa na serikali ya kuzuia matumizi ya majengo ambayo bado yanaendelea na ujenzi, jambo linalohatarisha maisha ya watu.
Hali hiyo imeonekana katika mitaa mbalimbali ya katikati ya jiji la Dar es Salaam, ambapo maghorofa mengi ambayo ujenzi wake haujakamilika, yanatumika kwa kufunguliwa ofisi na maduka huku ujenzi ukiendelea.
Machi 11 mwaka 2010, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisimamisha ujenzi wa jengo la ghorofa saba katika kiwanja namba 8/33, kilichoko mtaa wa Swahili na Mafia, Kariakoo, kutokana na kuwa na mpasuko uliotishia usalama.
Lukuvi alisema hatua hiyo inatokana na mapendekezo ya timu iliyokagua jengo hilo, ambayo ilihusisha wahandisi wa Manispaa ya Ilala na wa Sekretarieti ya Mkoa, ambayo ilibaini kuwepo kwa nyufa kwenye ghorofa ya kwanza, zinazosadikiwa zilitokana na msingi kutohimili uzito wa jengo hilo.
Pia alizuia kutumika kwa majengo ambayo bado hayajakamilisha ujenzi wake kwa sababu yanaweza kuhatarisha usalama wa watu.
Alisema kutokana na hatari inayoweza kusababishwa na kuanguka kwa jengo hilo, serikali imeamua kufunga barabara ya mtaa wa Mafia kuanzia makutano ya mtaa wa Nyamwezi mpaka makutano ya mtaa wa Sukuma.
Alisema mtaa wa Swahili pia utafungwa kuanzia makutano ya mtaa wa Mkunguni na Swahili mpaka makutano ya mtaa wa Kariakoo na Swahili.
Baadhi ya wafanyakazi wa maduka hayo wameliambia Uhuru kuwa, wanalazimika kuendelea kufanya kazi katika mazingira hayo ambayo ni hatarishi kwa sababu ya ukosefu wa ajira.
Walisema ni hatari kufanya biashara katika ghorofa ya chini huku juu ujenzi ukiendelea kwani jambo lolote linaweza kutokea, ikiwa ni pamoja na kuangukiwa na ukuta au matofali.
Rajab Mwita, ambaye anafanyakazi katika duka la simu  katika jengo ambalo halijakamilika, alisema wanafanya kazi katika mazingira magumu.
Mwaka jana jengo la ghorofa 16 katika mtaa wa Indira Gandhi katikati ya Jiji la Dar es Salaam, liliporomoka na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 30. 
Jengo hilo si la kwanza kuporomoka jijini Dar es Salaam. Miaka ya hivi karibuni, jengo la Chang’ombe Village katika Manispaa ya Temeke, ambalo lilikuwa la ghorofa  nne, liliporomoka na kuua watu wanne.
Pia jengo lingine la ghorofa 10 katikati ya Jiji liliporomoka na kuua watu watatu.
Mkuu wa wilaya ya Ilala, ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mushi, alipoulizwa na Uhuru kuhusu kuwepo kwa maghorofa ambayo yanatumika huku ujenzi ukiendelea, alisema atazungumza na Mkurugenzi wa Jiji kisha alitalitolea ufafanuzi suala hilo.

1 comments:

  1. Serekari ifate sheria ndio tutanyooka
    waache kulalamika mpaka wachoke
    ujenzi holela ufutwe mpaka mabondeni

    ReplyDelete