Wednesday, 2 July 2014

JK atuma salamu za rambirambi kifo cha Nkwabi Ng’wanakilala


Na Mwamvua Mwinyi
RAIS Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwandishi wa habari mkongwe na mhadhiri wa  Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Nkwabi Ng’wanakilala.
Ng’wanakilala alifariki dunia Juni 27, mwaka huu katika hospitali ya rufani Bugando, jijini Mwanza, baada ya kusumbuliwa na figo.
Katika salamu zilizotumwa  kwa Mkuu wa chuo hicho, Askofu Trcisius Ngalalekumtwa, Rais Kikwete, alisema kifo hicho kimelinyang’anya taifa mwana taaluma mahiri wa habari na mtumishi hodari.
Alisema sifa hizo alizipata na zilithibitika katika nafasi ambazo Ng’wanakilala alizishika wakati wa uhai wake.
ìAlithibitisha sifa hizo kwenye nafasi ya Ukurugenzi wa Idara ya Habari, kwenye Ukurugenzi wa Redio Tanzania Dar Es Salaam (RTD) na kwenye Ukurugenzi wa Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA),” alisema Kikwete katika salamu zake.
Ng’wanakilala, aliyefariki dunia wiki iliyopita alizikwa  juzi, nyumbani kwake, Kibamba wilayani Kisarawe mkoani Pwani.
Mapema, mtoto wa marehemu, Fumbuka Ng’wanakilala, akimzungumzia wasifu wa marehemu, alisema  baba yake alipata shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1972, alisoma kozi ya taaluma ya uandishi wa habari kwenye Chuo cha London School of Journalism nchini Uingereza.
“Pia baba aliwahi kusomea na kupata stashahada ya elimu ya watu wazima kutoka Chuo Kikuu cha Manchester, nchini Uingereza mwaka 1974.”
“Mwaka 1983 Ng’anakilala alihitimu kwenye chuo hicho na kupata shahada ya uzamili na kati ya 1983-84, baadaye alipata shahda za uzamivu katika Chuo Kikuu cha Tampere, nchini Finland,î alisema.
Alisema mbali na kushika nafasi za juu katika baadhi ya taasisi nchini, baba yake pia aliwahi kujiunga na Jumuia ya Nci za Kusini mwa Afrika akifanya na kufanya kazi nchini Botswana.
Ng’wanakilala alistaafu kwenye ajira ya serikali mwaka 1997.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru