Wednesday, 2 July 2014

Kichanga cha miezi sita chabakwa Butiama


Na Ghati Msamba, Butiama
MTOTO mwenye umri wa miezi sita (jina linahifadhiwa) amebakwa katika kitongoji cha Nyarufu, kijiji cha Murangi, wilayani Butiama, mkoani.
Habari zinasema kuwa kichanga hicho kilibakwa na mtu asiyejulikana.
Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya mtoto wa mwaka 1 na mwingine wa miezi 6 kubakwa wilayani hapa.
Akizungumza katika zahanati ya Murangi, mama wa mtoto huyo, Robby Mwita (18), alisema juzi saa 2 asubuhi,  alimwacha mtoto wake nyumbani akiwa na shemeji yake, aliyemtaja kwa jina la Manyama Sirira (25) na  aliporejea alimkuta pekee  akilia kwa uchungu.
Robby alisema shemeji yake alikuwa ameshaondoka, lakini mtoto alikuwa akilia na kushika sehemu za siri, baada ya kumchunguza alikuta anavuja damu na akiwa amechanika.
Alisema aliwaita majirani na kuongozana nao hadi kwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Nyarufu, Ebson Majinge, baadaye kwa Mwenyekiti wa kijiji cha Murangi ili awaandikie barua ya kwenda kupata matibabu.
Robby alisema walipata barua na kwenda hospitali, lakini mgambo hawakuweza kumsaka mtuhumiwa baada ya kukosekana kwa fedha za kuwawezesha kufanya kazi.
Mama wa mtoto huyo alilalamika mumewe kutompa ushirikiano kwa vile mtoto huyo si wake. “Mwanaume huyu alinioa mtoto huyu akiwa na miezi mitatu...nilizaa na mwanaume mwingine,” alisema.
Alisema huenda mume wake ameshindwa kutoa ushirikiano kutokana na aliyefanya tukio hilo kuwa ni ndugu yake.
Mganga wa zahanati ya Murangi, Josephat Musagasa, alisema katika vipimo na uchunguzi wa awali, wamebaini mtoto huyo kubakwa.
Alisema uchunguzi zaidi unafanywa kuhusiana na afya ya mtoto.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru