Tuesday, 1 July 2014

TAG kugawa vyandarua 8,550


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
KANISA la Tanzania Assemblies Of God (TAG), linatarajiwa kugawa vyandarua 8,550 vyenye thamani ya sh. milioni 135 katika hospitali 34 na vituo vya afya 83 kwenye mikoa ya Njombe, Mbeya na Rukwa.
Vyandarua hivyo vitaanza kugawiwa katika hospitali na vituo vya afya vyote vya serikali, taasisi za kidini na binafsi.
Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali, aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kugawa vyandarua hivyo katika hospitali ya Rufani Mbeya, ikiwa ni maadhimisho ya Jubilei ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1939.
Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo yatakayofanyika Julai 13, mwaka huu, atakuwa Rais Jakaya Kikwete.
Dk. Mtokambali alisema baada ya uzinduzi huo wa kugawa vyandarua, viongozi wa kitaifa wa kanisa la TAG, makamu askofu mkuu, katibu mkuu na maaskofu wa majimbo ya kanisa hilo yaliyopo katika mikoa hiyo, watasambaza vyandarua katika maeneo mengine.
“Kanisa la TAG kama sehemu ya jamii linatambua ukubwa wa tatizo la ugonjwa wa malaria hasa kwa kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano,” alisema Dk. Mtokambali.
Aliongeza kuwa pamoja na kutoa huduma ya kiroho, wanaunga mkono juhudi za serikali katika kufikia malengo ya milenia kwenye mapambano dhidi ya malaria.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru