Tuesday 1 July 2014

Wawili mbaroni kwa mauaji ya sista Dar


EVA MBESELE NA RACHEL KYALA
JESHI la Polisi limewakamata watu wawili wanaotuhumiwa kuhusika na kifo cha Mtawa wa Kanisa Katoliki, Clesencia Kapuri (50) aliyeuawa Juni 23, mwaka huu, huko Ubungo Kibangu, Dar es Salaam.
Majambazi hao  licha ya kuhusishwa  na tukio hilo na kupora sh. milioni 20, pia walikuwa wakitafutwa kwa muda mrefu kwa tuhuma za tukio la uporaji wa fedha katika benki ya Barclays tawi la Kinondoni. 
Hata hivyo, kinara wa ujambazi katika tukio la uporaji kwenye benki hiyo, Leonard Mollel, hajatiwa mbaroni na msako mkali unaendelea. Mollel anatajwa kuwa ni mume wa kigogo mmoja wa Barclays, ambaye tayari amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za wizi wa mamilioni ya shilingi.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akizungumza jana jijini Dar es Salaam, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Manase Ogenyeka (35) maarufu kwa jina la Mjeshi, mkazi wa Tabata Chang’ombe na Hamis Ismail, (Carlos), ambaye ni mfanyabiashara, mkazi wa Magomeni Mwembechai.
Majambazi hao walishirikiana na wenzao sita ambao ni Beda Mallya (37), Michael Mushi (Masawe), Sadick Kisia (32), Elibariki Makumba (30), Nurdin Suleiman (40) na Mrumi Salehe (Chai bora).  
Kamanda Kova alisema watuhumiwa wawili kati ya hao sita, Elibariki Makumba, na Mrumi Salehe walikamatwa baada ya kufanya jaribio la kughushi hati na kuzitumia kuombea kazi katika kampuni binafsi ya ulinzi ya Instant Security Services iliyopo Msasani, Dar es Salaam.
“Lengo lao ilikuwa ni kujifanya wanalinda kupitia kampuni hiyo ili baadaye waweze kutenda uhalifu kwa urahisi huku wakishirikiana na mtandao wao,” alisema.
Vilevile Kamanda kova alizitaka kampuni za ulinzi kulishirikisha Jeshi la Polisi pindi zinapotaka kuajiri wafanyakazi ili kuchukua vipimo mbalimbali ikiwemo alama za vidole, DNA pamoja na kupigwa picha.
Alisema uchunguzi wa polisi umegundua kuajiriwa kwa wezi kwenye kampuni nyingi za ulinzi, hasa katika jiji la Dar es Salaam.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru