Thursday, 12 March 2015

Achaneni na wapinzani, hawana serikali- Nape


WANANCHI wametakiwa kuwa macho na baadhi ya vyama, ambavyo lengo lao ni kuwagawa wananchi kwa maslahi yao.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi,  Nape Nnauye, alipozungumza na wakazi wa kijiji cha Itolwa wilayani Chemba.


Alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya vyama kwenda kwa wananchi kuwalaghai kuwa vingeweza kufanya mabadiliko ya hali zao za kimaisha endapo wagombea wake watachaguliwa.
Nape alisema watu hao ni wadanganyifu kwani wanapochaguliwa, hawaonekani kutokana na kutokuwa na serikali.
“Muwe macho na hawa watu wanaokuja kuwalaghai kuwa wana uwezo wa kufanya mambo mbalimbali. Ukweli ni kwamba  hawana serikali, sasa watatekeleza hayo kutoka wapi? Alihoji Nape.
Aliwataka wakazi hao kukipenda Chama cha Mapinduzi na kuachana na watu hao kwani nia yao ni kuigawa nchi vipande vipande.
“Ukiona kinaelea uje kimeundwa, sasa kama nchi hii imefikia hapa, lazima kuwe na aliyeunda na huyo si mwingine ni CCM,” alisema Nape.
Aliongeza kuwa sehemu nyingi, ambazo wapinzani wamepata uongozi kumekuwa na migogoro mingi kutokana na amani kutoweka.
Alitoa mfano wa Mji wa Arusha, ambao awali ulikuwa ni mji wa kitalii wenye sifa nyingi, lakini baada ya kuongozwa na wapinzani, sasa umekuwa mji wa maandamano na migogoro.
“Nawaomba wananchi kushikamana na CCM kwani ndicho chama pekee kinachoweza kuwasaidia katika kuondoa kero zenu na si kingine,” alisema Nape.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru